Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (Kulia,) akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Tigo Mawasiliano Innocent Rwetabura (Kushoto) wakati alipotembelea kampuni hiyo leo jijini Dar es Salaam.


SERIKALI imewahakikishia watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini kwamba itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha kukuza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, ili kukuza tija kwenye sekta ya mawasiliano nchini.


Hayo yalibainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Moses Nauye katika ziara yake kwa kampuni tatu za simu nchini za Tigo, Vodacom na Airtel aliyoifanya leo Jumatatu Tarehe 24 Januari 2022.


Waziri Nape amesema, Nia ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa, wawekezaji wanawekewa katika mazingira rafiki yatakayowawezesha kukuza tija katika uwekezaji wao.


“Katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, serikali ipo tayari kuboresha mazingira yakiwemo haya mazingira ya kazi yenu. Ninyi ni wadau wetu sisi ni wadau wenu, tunaweza kuzungumza, tukaaminiana, tukatengeneza mazingira mazuri zaidi; hayo mazingira tunayotaka tuyatengeneze, yatusaidie na yawashawishi muwekeze zaidi.” Amesisitiza Waziri Nape.


“Tunao watanzania tunaowahudumia, sisi kama serikali na ninyi kama ‘operators’; wale tunaowahudumia wanatutegemea kutoa huduma nzuri, sisi huku tuwe na mahusiano mazuri ili huduma tunayoitoa iwe bora.” Waziri amesisitiza na kuongeza alipozungumza na ujumbe wa Menejimenti na Bodi ya kampuni ya Vodacom Tanzania.


Amesema, mchango wa wadau hao ni mkubwa katika uchumi wa nchi na wamewekeza kwa fredha nyingi, wanalipa kodi, wametoa ajira nyingi kwa vijana wa kitanzania na huduma zao zinasaidia huduma nyingine katika jamii, Hivyo Serikali imetoka ofisini na kwenda kuwasikiliza changamoto zao na wapi wawasaidie ili kuleta matokeo chanya zaidi na watapitia sheria, sera na miongozo katika kufanikisha hilo zaidi.


Katika ziara hiyo, Waziri Nape alipata fursa ya kuwasikiliza watoa huduma za mawasiliano ya simu kisha kufafanua kuwa, Serikali imepokea changamoto kadhaa walizoainisha katika utoaji huduma na mazingira ya uwekezaji ili kuona namna itakavyozifanyia kazi na kuhakikisha zinapatiwa suluhu


Katika ziara hiyo Waziri alisisitiza umuhimu wa kampuni za simu nchini kuhakikisha zinaboresha huduma wanazotoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha ubora wa usikivu wa simu na matumizi ya data hasa kwa watumiaji wa intaneti.


“Tunaweza kuwa na mapungufu ya hapa na pale, sasa hayo mapungufu tuyaondoe hii ni meseji ya muhimu sana.” Ameeleza Nape.


Wakati wa ziara hiyo kwa nyakati tofauti Waziri alipokea taarifa za maboresho kwenye sekta ya mawasiliano kutoka kwa kampuni zote ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni kuondoka miundombinu chakavu na kubadilisha mipya sanjari na kuhuisha teknolojia ikiwemo inayowezesha upatikanaji wa huduma kwa wateja kwa urahisi kwa kutumia programu tumizi zilizoainishwa.


“Tumejipanga kuhakikisha tunatoa huduma zenye ubora kwa wateja wetu na tutalisimamia hilo.'' alisisitiza Beatrice Singano Afisa Habari Mwandamizi wa kampuni ya Airtel.


Wakati wa majumuisho Waziri Nape ameeleza umuhimu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujenga mahusiano mazuri na watoa huduma ili kuhakikisha utoaji huduma za mawasiliano kupitia kampuni hizo unakuwa bora siku hadi siku na kuongeza kuwa Wizara yake itaona namna ya kuweka mazingira bora zaidi ya ukuzaji sekta ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupitia miongozo muhimu inayoilinda sekta pana ya mawasiliano nchini.


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akipata maelekezo ya namna huduma kwa wateja zinavyotolewa katika kampuni ya mawasiliano ya Tigo, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akipata maelekezo ya namna huduma kwa wateja zinavyotolewa katika kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (katikati,) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Sitholizwe Mdlalose (katikati) na Mkurugenzi wa Vodacom Foundation Bi. Roselyn Mworia, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC Jaji mstaafu Thomas Mihayo mara baada ya kuhitimisha ziara katika ofisi ya makao makuu ya kampuni hiyo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akipokelewa Afisa Habari Mwandamizi wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Beatrice Singano Afisa Habari Mwandamizi wa kampuni ya Airtel leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza na Menejimenti ya kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania, Leo jijini Tanzania.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...