Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMLAKA ya Bandari Tanzania( TPA) imeagizwa kuhakikisha katika nafasi 600 za ajira walizoombea kibali Serikalini wanatoa kipaumbele kwa wahitimu wa Chuo Cha Huduma za Bandari ( Bandari College).
Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete wakati wa mahafali ya 20 ya Chuo cha Bandari kilichopo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 709 wamehitimu masomo yao kwa ngazi mbalimbali za kitaaluma.
Akizungumza zaidi Mwakibete amesema kwamba ni vema wahitimu wa Chuo hicho wakapewa kipaumbele na TPA kwani wanatambua wameomba kibali kwa ajili ya kuajiri watumishi,hivyo lazima kipaumbele kiwe kwa wahitimu wa Chuo hicho.
"Hakutakuwa na maana uwepo wa chuo hicho kama nafasi za kazi kwenye Mamlaka ya Bandari wanapewa watu wengine huku wahitimu wa Chuo hicho wakiachwa mtaani.
Ni vema TPA itoe kipaumbele kwa wahitimu wa Chuo hicho iki kukipa hadhi na kukiongezea sifa na hili ni agizo kwenu Mamlaka, kunapotokea nafasi za kazi katika ngazi ya elimu ambayo inayolewa hapa chuoni basi product la chuo hiki lipewe nafasi ya Kwanza.
"Kabla ya kuangalia watu wengine nje ya Chuo hiki, na hii ndio ilikuwa sababu ya awali ya kuanzishwa kwa chuo hiki," amesema na kusisitiza Seriki kupitia Mamlaka ya bandari wataendelea kukiboresha na kukiimarisha chuo hicho iki kikidhi soko.
Kuhusu changamoto katika chuo hicho,amesema mojawapo ni ya uhaba wa majengo,hivyo ametoa maagizo kwa Kamati maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia mazungumzo ya pande mbili Kati ya uongozi wa chuo hiki na Chuo cha Utalii kufanya kazi zake katika muda ukiopangwa ili maamuzi yake yafike ngazi ya Wizara Kwa ajili ya utekelezaji.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamisi, pamoja na mambo mengine amesema kwa sasa Chuo cha Bandari kinazidi kupanuka na hivyo kuwa na uhitaji wa kuongeza miundombinu yake.
Aidha amesema chuo cha Bandari kinafanyiwa mageuzi ya kitaaluma kutokana na juhudi za serikali za kuboresha uwepo wa bandari nchini huku akieleza imeunda kamati maalumu kufuatilia suala la Chuo cha Utalii kuchukua majengo ya Chuo hicho na ripoti hiyo itawasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya hatua zaidi.
Mkurugenzi huyo wa TPA amesema kutokana na uamuzi uliofanyika mwaka 2001 wa kugawanya takribani asilimia 70 ya eneo la chuo cha Bandari na kukabidhiwa ka chuo cha utalii, asilimia 30 iliyobaki ya chuo hicho imezidi kuwa finyu.
“Napenda kuwataarifu kuwa suala hili limeundiwa kamati ikihusisha vyuo vyote viwili ili kujadili uwezekano wa kurejesha majengo ya chuo cha Bandari. Watalaamu hawa wataandaa andiko la ushauri na kuliwakilisha kwa Waziri wa Uchukuzi ambaye atatoa mrejesho wake,” alieleza Hamisi na kusisitiza uwepo wa chuo hicho ni muhimu katika sekta ya bandari nchini,hivyo wataendelea kuweka mikakati itakayoendelea kukiboresha na kuimarisha.
Wakati huo huo Mkuu wa Chuo hicho, Dk.Lufunyo Hussein alielezea mageuzi makubwa ya kukiboresha chuo hicho kuwa ni pamoja na mpango wa kuanzisha kozi ya shahada ambapo kinatoa tu kozi za cheti na diploma pamoja na kuanzisha maabara maalumu ya kisasa ya masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika masuala ya bandari.
Amesema katika eneo la Shahada wako kwenye hatua ya kuandaa mitaala kupitia kukusanya maoni ya wadau ili shahada itakayotolewa ijibu mahitaji ya soko husika. Kuhusu maabara tunataka tuwe kituo maalumu cha Tehama na mifumo yote ya bandari. Watalaamu wa kuanzisha maabara hiyo wanao wa kutosha.
Pamoja na hayo, amesema kuna mipango mingine ikiwemo ya kufanya utafiti, kuboresha majengo ya chuo hicho ambayo mengi yamechakaa zikiwemo karakarana.
Ameongeza ema chuo hicho, tayari kimesimika mitambo ya kisasa ya ufundishiaji kwa vitendo miwili ambayo kila mmoja una gharimu takribani kiasi cha Sh.bilioni 1.2 na matarajio ni kuongeza mtambo mmoja ili kuzalisha wahitimu wenye weledi na utaalamu wa kutosha bandarini.
Sehemu ya wahitimu wa Chuo Cha Bandari mkoani Dar es Salaam wakiwa makini kumsikiliza mgeni rasmi hayuko pichani wakati wa sherehe za mahafali ya Chuo hicho
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...