Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari mawili aina ya Toyota Double Cabin yaliyokabidhiwa  tarehe 03/02/2022 Kwa wakuu wa Campasi za Wakala wa vyuo vya Mifugo Tanzania. Kutoka kulia ni Mtendaji mkuu wa LITA Dkt.Pius Mwambene,Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya LITA Prof.Malongo Mlozi.
magari mawili aina ya Toyota Double Cabin yaliyokabidhiwa  tarehe 03/02/2022 Kwa wakuu wa Campasi za Wakala wa vyuo vya Mifugo Tanzania

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Tixon Nzunda akiteta jambo na Mkurugenzi wa Utafiti Mafunzo na Ugani DRTE Dkt. Anjello Mwilawa (kushoto), nyuma ya katibu mkuu ni Mweyekiti wa Bodi ya Ushauri LITA Prof.Malongo Mlozi na Mtendaji Mkuu wa LITA Dkt.Pius Mwambene. 


KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Tixon Nzunda ametoa wito kwa Wakala ya vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuimarisha mifumo ya utafiti na ushauri kwa wafugaji, sambamba na kuongeza ubunifu kwa kuanzisha huduma mtandao zenye kuwaunganisha pamoja na wafugaji, wadau wa sekta ya mifugo na taasisi zingine za Umma na binfasi.


Nzunda ametoa wito huo  (03.02.2022) Mkoani Morogoro wakati akizungumza na Bodi ya wakala hiyo na Maafisa wasimamizi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya mifugo kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

"Anzisheni mifumo imara ya usimamizi na uwajibikaji, huu utendaji wa kuamka asubuhi unaenda  kazini kama kawaida, umepitwa na wakati, unachelewesha maendeleo, kwasasa tuanze kupimana kwa Mikataba ya utendaji kazi ili tuanze kuona utendaji wa kila mmoja wetu jinsi anavyotekeleza majukumu aliyopewa, kama umefanikiwa, sawa, na kama amekwama tatizo ni nini mpaka  umekwama? hii itatupa nafasi ya kuhoji kama unastahili kuendelea  na nafasi uliyonayo. alisema Nzunda"

Nzunda amesisitiza kuwa Serikali inahitaji kuona matokeo chanya kupitia Sekta ya Mifugo kwa kuimarisha na kusogeza huduma kwa wananchi ikiwemo kuendelea kupanua wigo wa huduma za ugani kwa wafugaji ili kuondokana na ufugaji wa mazoea usioleta tija kwa wafugaji walio wengi.

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo ni muhimu itekeleze jukumu la kuwafikia wafugaji  kwa kutumia rasilimali kidogo waliyonayo ili kuleta matokeo makubwa.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya wakala hiyo Prof. Malongo Mulozi, amesema kuwa LITA   wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa usafiri wa kuwapeleka wanafunzi katika masomo ya Vitendo pamoja na kuwafikia wafugaji.

 Aidha, ametaja changamoto nyingine kuwa ni  uchakavu wa miundombinu ya kufundishia na uhaba wa nyumba za watumishi ambapo alibainisha kuwa pindi fedha itakapopatikana ukarabati na ujenzi wa nyumba hizo utaanza mara moja.

Vile Vile Prof. Mlozi amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa changamoto hizo, moja ya mikakati ya Taasisi hiyo ni kuzalisha na kuandaa vijana wenye uwezo wa kujiajiri kupitia Sekta ya Mifugo na kwamba kila kituo  kina mradi wake wa mapato kulingana na hali ya mazingira kilipo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo,  Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa majukumu  makubwa ya Taasisi yake  ni pamoja  na kutoa mafunzo ya muda mrefu na Mfupi, Kutoa huduma za Ushauri wa kitalaam wa Mifugo, kufanya tafiti na tathimini pamoja na kuzalisha na kutunza Mifugo ya kufundishia.

Dkt. Mwambene amesema kuwa kwasasa vyuo hivyo vinawanafunzi zaidi ya 4,000 ukilinganisha na wanafunzi 700 waliokuwepo  wakati wanaanza mafunzo hayo  miaka kumi iliyopita, na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) imeendelea kuhimiza  kufanyika maboresho katika miundombinu ikiwa ni pamoja na kusimamia ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika vyuo hivyo.

Pia Dkt. Mwambene ametoa wito kwa  wadau mbalimbali kujitokeza na kuingia ubia na wakala hiyo ili kusaidia uwekezaji wa  mafunzo kwa wanafunzi hao.

Mazungumzo baina ya Nzunda na Watendaji wa Wakala hiyo  yalienda  sambamba na makabidhiano ya magari mawili aina ya "Toyota Double cabin" kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi  wa taasisi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...