Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , ameishauri Mahakama  kuandaa mipango bora  inayolenga nyanja za kimaisha na kujenga ufanisi katika uzalishaji ili kukuza shughuli za uwekezaji na kuimarisha uchumi nchini.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo huko Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar mara baada ya  matembezi na mazoezi ya viungo ikiwa ni shamra shamra za kuelekea kilele cha siku ya Sheria duniani inayotarajiwa Kufanyika Jumatatu Februari 7 mwaka huu.

Amesema kuwa sekta ya sheria kama zilivyo fani nyingine za kitaalamu, inahitaji kuzingatia uwiano na nyanja nyingine za kimaisha zikiwemo za biashara na uwekezaji  ili kusaidia kukuza uzalishaji kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Othman amesema, kama inavyoelekeza Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Mwaka huu isemayo 'Usimamizi wa Haki ni msingi wa maendeleo ya  kiuchumu na kijamii, hivyo si vyema kwa wadau wa sheria kuegemea upande huo pekee na kusahau sehemu ya maisha katika jamii.

Aidha, Mhe. Othman amependekeza hatua ya Mahakama kuanzisha  Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara ili kusaidia kujenga imani kwa wawekezaji na wafanyabiashara, sambamba na kuendeleza vyema sekta ya uwekezaji itakayosaidia kujikwamua kiuchumi.

Naye Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amesema kufanyika kwa shamrashamra hizo zilizoanza tangu tarehe 1 Februari mwaka huu, kwa harakati mbali mbali, kunasaidia kukuza uelewa na ukaribu baina ya wadau wa sheria na jamii.

Shamrashamra hizo zimeambatana na matembezi kuanzia Jengo la Mahakama Kuu ya Vuga kupitia Barabara ya Michenzani na Kariakoo Unguja, kabla ya mazoezi ya viungo yaliyowahusisha pia Viongozi, Wanasheria, Majaji, Bendi ya Jeshi la Polisi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Viongozi waliojumuika katika shamrashamra hizo ni pamoja na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa, Naibu Kadhi Mkuu, Sheikh Hassan Othman Ngwali na Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...