Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 27 Februari 2022 amekutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa Nigeria Prof. Yemi Osinbajo, mazungumzo
yaliofanyika Jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amemkaribisha Prof Osinbajo nchini Tanzania na kuishukuru nchi ya Nigeria kwa ushirikiano uliopo na Tanzania tangu enzi za kupigania uhuru wa nchi za Afrika.
Amesema nchi ya Tanzania na Nigeria zimeendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta za kifedha kupitia United Bank of Africa pamoja na uwekezaji ikiwemo kampuni ya uzalishaji Saruji ya Dangote inayozalisha saruji kwaajili ya Tanzania na nchi jirani.
Dkt. Mpango amemueleza Makamu wa Rais wa Nigeria kwamba nchi hizi mbili bado zina nafasi ya kushirikiana katika masuala mengi zaidi na kumueleza ipo haja ya kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya ushirikiano itakayoharakisha ushirikiano katika biashara, utalii, elimu pamoja kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo za kodi.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Tanzania inaendelea na jitihada za kufufua uchumi uliothiriwa na Uviko 19 katika sekta mbalimbali. Amesema serikali inayoongozwa na Rais samia Suluhu Hassan inaendeleza miradi mikubwa ilioasisiwa na Awamu ya Tano ikiwemo ya nishati katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na miundombinu ikiwemo Reli ya kisasa (SGR) pamoja na kuanzisha miradi mipya itakayoimarisha uchumi pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Nigeria Prof. Yemi Osinbajo ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kupokea uwekezaji kutoka nchini Nigeria na kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara kwa wawekezaji hao. Amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Nigeria ni wakindugu ulioanza muda mrefu tangu 1962 ulipoanzishwa ubalozi wa Nigeria Nchini Tanzania.
Aidha Prof Osinbajo ameongeza kwamba kinachohitajika kwa sasa ni kufanya kazi pamoja, kujivunia rasilimali zilizopo na kwa kutumia viongozi imara waliopo madarakani katika kujiletea maendeleo. Amesema serikali ya Nigeria katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania itafuatilia makubaliano yoyote yaliokwama baina ya nchi hizi mbili ili kupata ufumbuzi wa haraka. Ameongeza kwamba nchi hizi mbili zinapaswa kushirikiana kuliko ilivyo sasa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Nigeria Prof. Yemi Osinbajo, mazungumzo yaliofanyika Jijini Arusha leo tarehe 27 Februari 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Nigeria Prof. Yemi Osinbajo mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliofanyika Jijini Arusha leo tarehe 27 Februari 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...