Shirika
la Reli Tanzania laendelea na Wiki ya TRC kwa kufanya ziara jijini
Mwanza katika vyombo vya habari nchini ambako reli imepita, Februari
2022.
Lengo
la Wiki ya TRC ni kuuhabarisha umma kuhusu shughuli mbalimbali za
Shirika ikiwemo huduma za usafiri wa abiria na usafirishaji mizigo,
masuala ya usalama wa reli halikadhalika Miradi ya kimkakati
inayosimamiwa na Shirika ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR
ambao unaendelea kwa wamau ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza katika
vipande vya Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora, Isaka –
Mwanza na Makutupora – Tabora ambacho mkataba wake umesainiwa hivi
karibuni Disemba 2021.
Akiwa
katika Shirika la Utangazaji Nchini – TBC Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Reli Tanzania alieleza kuwa “Tuko kwenye Wiki ya TRC na lengo kubwa ni
kuwahabarisha watanzania kuhusu nini tunafanya, uendeshaji wa treni na
ujenzi wa miundombinu, tulifanya mkutano na waandishi wa habari na sasa
tunaendelea na ziara kwenye vyombo vya habari”
Wiki
ya TRC huadhimishwa na Shirika kila mwaka ambapo kitengo cha Habari na
Uhusiano kwa kushirikiana na Idara nyingine za Shirika huandaa ziara
katika vyombo vya Habari katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro,
Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro
na Arusha.
“Hii
reli imepita mikoa 16, kwahiyo wananchi ndio walinzi wa kwanza wa reli
ukizingatia kwamba zimetumika zaidi ya trilioni 14.7 kwenye mradi wa SGR
ambazo ni pesa za wananchi hivyo tunawaelimisha katika Wiki hii ya TRC
ili wajue kuwa reli hii ni mali yao” alisema Kadogosa
Akizungumza
kuhusu majaribio ya treni za kisasa za SGR Ndugu Kadogosa alieleza kuwa
majaribio ya njia pamoja na mifumo mingine ya reli ya kisasa yalianza
mwezi Oktoba 2021 na yanaendelea, kilichobaki ni majaribio kwa kutumia
treni ambazo zinatarajiwa kuwasili nchini Aprili 2022.
“Majaribio
tumeanza tangu Oktoba 2021, tunafanya majaribio ya njia, madaraja na
mifumo ya umeme na hatua ya mwisho itakuwa ni kupitisha treni ambayo
itafanya majaribio ya mifumo yote, majaribio hayo yataanza mara baada ya
treni kuwasili mwishoni mwa mwezi Aprili 2022” alisema Kadogosa
Kadogosa
aliongeza kuwa “Mkandarasi naye anaendelea na majaribio kwa kutumia
treni yake inayotumia Dizeli lakini tarehe 17 Februari 2022 ataleta
kichwa kinachotumia umeme na ataanza majaribio ya umeme”
Mkurugenzi
Mkuu katika ziara yake katika vyombo vya Habari mkoani Dar es Salaam
alieleza baadhi ya faida na sababu za utekelezaji wa mradi wa reli ya
kisasa kuwa ni kuunganisha ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na Afrika
kwa ujumla kwakuwa mradi huu uliwekwa kwa makubaliano baina ya nchi za
Afrika kwa lengo la kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Reli
ina historia kubwa katika taifa, ni zaidi ya miaka 100, mjerumani
alijenga, akaja muingereza akajenga kidogo lakini baada ya uhuru Hayati
Mwalimu Nyerere alijenga, hivi sasa tunazungumzia reli ya kisasa
(standard gauge), hii ni kwamba unaweza ukaenda, Kigali, Bujumbura,
Uganda na ukarudi hii ndiyo maana ya ‘Standard’ kwa maana ni reli yenye
viwango vinavyotumika karibu Dunia nzima” aliongeza Kadogosa.
Mkurugenzi
Mkuu TRC ameeleza kuwa mradi wa SGR unaendelea vizuri ambapo kwa
kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) kimefika 95%, kipande cha
Morogoro – Makutupora (km 422) kimefika 81%, kipande cha Isaka – Mwanza
(km 361) kimefika 4% huku kipande cha Makutupora – Tabora (km 361) kipo
katika hatua za awali za maandalizi kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi
na kuanza ujenzi.
Kwa
upande wa behewa na vichwa vya treni Kadogosa amesema kuwa Serikali
imeagiza behewa za kubeba abiria, treni zenye vichwa mbele na nyuma
(EMU) ambazo mara nyingi zinakwenda masafa mafupi, behewa za kawaida
ambazo zitakuwa kwa ajili ya masafa marefu ambazo ziko 59, vichwa 17,
pia Serikali imeagiza behewa 30 za gorofa na vichwa viwili vya treni
ambavyo vitaanza kwa ajili ya majaribio.
Aidha,
Kadogosa amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa maamuzi haya, ndani ya muda
mfupi ameweza kufanya mambo makubwa, kipindi anapokea uongozi tulikuwa
tunajenga vipande viwili lakini mara baada ya kuanza uongozi wake
tumeona tayari vipande viwili vimeshatiliwa saini kwa ajili ya ujenzi.
Wiki
ya TRC inaendelea ambapo hivi sasa timu ya mawasiliano ikiongozwa na
Mkurugenzi Mkuu Masanja Kadogosa iko Mwanza na baadaye itaendelea na
ziara hiyo katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma,
Morogoro na kuhitimisha katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Shirika
linawaomba wananchi kufuatilia Wiki hii katika vyombo vya Habari pamoja
na mitandao ya kijamii ili waweze kupata taarifa na elimu sahihi kuhusu
shughuli zinazofanywa na shirika sambamba na masuala ya usalama wa reli
ili miundombinu ya reli iendelee kuwa salama kwa matumizi ya sasa na
kwa vizazi vijavyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...