Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 03 Februari, 2022 amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (International Finance Cooperation – IFC) Bw. Makhtar Sop Diop Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Diop amempongeza Mhe. Rais Samia kwa mafanikio aliyoyapata katika Serikali ya Awamu ya Sita kutokana na utendaji mzuri wa kazi katika kuwaletea maendeleo watanzania, ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi na kusimamia mfumuko wa bei nchini Tanzania.  

Aidha, Bw. Diop amemfahamisha Mhe. Rais Samia kwamba Shirika hilo litaendelea kushirikiana na sekta binafsi nchini Tanzania, pamoja na kuangalia namna ambayo wanaweza kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga na kuwawezesha kiuchumi wanawake wanaofanya kazi katika sekta binafsi.

Bw. Diop amesema eneo jingine ambalo IFC ingependa kushirikiana na Tanzania ni kuimarisha sekta ya usafiri nchini hususan usafiri wa majini, kuwajengea uwezo wawekezaji katika miradi mikubwa ya ujenzi wa makazi pamoja na uwekezaji zaidi katika elimu na afya.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemshukuru Bw. Diop na ujumbe wake kwa kumtembelea na amewapongeza kwa kukuendelea kuunga mkono sekta binafsi na anatarajia kuwa wataendelea kuiunga mkono zaidi sekta hiyo.

Mhe. Rais Samia ameipongeza IFC kwa ushirikiano mkubwa inayoutoa kwa Tanzania katika kuunga mkono jitihada zake za maendeleo na kuihakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika hilo katika kutekeleza majukumu yake hapa nchini.

Aidha, Mhe. Rais Samia pamoja na mambo mengine amemueleza    Bw. Diop hatua mbalimbali zilizofikiwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya elimu, afya, barabara vijijini, usimamizi wa reli ya kisasa (SGR) pamoja na kutumia fursa za uchumi wa buluu. 

Jaffar Haniu
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

 

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji  wa International Finance Cooperation (IFC) Makhtar Sop Diop pamoja na Ujumbe alioambatana nao Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 03 Februari, 2022.

 





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji  wa International Finance Cooperation (IFC) Makhtar Sop Diop mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 03 Februari, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...