Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation ambayo inajishughulisha na masuala ya kijamii kwa niaba ya kampuni ya Vodacom Tanzania Plc, imeingia makubaliano na African Child projects (ACP) kuunganisha shule 50 nchini kwenye mtandao wa intaneti pamoja na kuzipatia vifaa vya kujisomea kidijitali ikiwemo kompyuta.

Makubaliano hayo yanalenga kuunganisha shule 50 ambazo ziko katika mikoa 10 nchini na kuonyesha njia endelevu kitaifa ya kuunganisha shule kidijitali. Mradi huu umebuniwa ili kuchangia jitihada za kutambua shule zenye uhitaji pamoja na kuziunganisha shule hizo na intaneti ili kupata suluhisho kwa wahitaji katika mazingira ambayo rasilmali ni finyu.

Akiongea wakati wa kusaini makubaliano hayo, Rosalynn Mworia, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation alisema, “dhamira yetu ni kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali kupitia teknolojia. Tuko tayari kutimiza wajibu wetu kwa kushirikiana na serikali na wadau wote wanaohusika ili kujenga mazingira wezeshi pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ili kutimiza malengo yetu ya kujenga jamii ya kidijitali nchini.”

“Tunaamini hii itasaidia nchi kwa kiwango kikubwa kufikia lengo la tisa endelevu la maendeleo (SDG9) ambalo linalenga kuongeza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa TEHAMA na kujitahidi kuleta upatikanaji wa huduma za intaneti kwa gharama nafuu kwa nchi zinazoendelea, Tunaimani kuwa kuwa elimu inauwezo wakuhakikisha Maisha ya mbeleni na hivyo tumewekeza katika sekta hiyo,” aliongeza Mworia.

Chini ya mkataba huu, Vodacom Tanzania Foundation, ikishirikiana na taasisi ya Vodafone Foundation, itagawa kompyuta 186, tablet 246 pamoja na uunganishwaji kwenye mtandao wa intaneti kwa mwaka mmoja kwa shule 50 nchini. Shule hizi ziko katika mikoa ya Kilimanjaro, Mara, Tabora, Katavi, Morogoro, Iringa, Ruvuma, Njombe, Kigoma na Tanga.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhandisi Samson Mwela, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA alisema, “misingi ya TEHAMA ina nafasi kubwa katika maendeleo na ukuaji wa kitaifa na hivyo kunahitajika mikakati na usimamizi madhubuti ili nchi iweze kufaidika na ukuaji wa TEHAMA. Katika mazingira ya sasa ya uchumi unaotegemea TEHAMA, ni muhimu kwa sekta zote zinazoendeshwa na TEHAMA ili kuweza kumudu mabadiliko yanayotokea nchini na duniani kwa ujumla. Ni furaha kubwa kuona sekta binafsi ikishirikiana na AZAKI kutimiza malengo na sera za kitaifa. Tunapongeza jitihada hizo.”

Mwela aliendelea kuelezea nia ya serikali ya Tanzania kuleta elimu ya kiwango bora iwezekanavyo kwa wananchi, “Katika ulimwengu wa sasa, upatikanaji wa huduma kidijitali unazidi kuwa muhimu katika utoaji wa maudhui ya elimu. Tunaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuaji wa mitandao haswa katika maeneo ya vijijini ili kuhakikisha tunatimiza malengo yetu na hivyo kuwanufaisha watanzania wote kwa matunda ya maisha ya kidijitali.”

Lengo kuu la mradi huu ni kuunganisha shule hizo na kuleta upatikanaji wa maudhui ya elimu bila gharama yeyote. Hivyo, mradi huu unaendana kikamilifu na malengo ya Vodacom Tanzania Foundation katika kuunganisha watanzania, kupata elimu na kujenga uwezo wa kidijitali kwa vizazi vijavyo. Zaidi, mradi huu utafungua jukwaa la elimu la Vodacom kwa shule 50 na wanafunzi takribani 42,291 pamoja na waalimu wao.

Aidha, chini ya makubaliano haya, wanafunzi watanufaika na maudhui ya bure yanayopatikana kupitia mfumo wa E-Fahamu unaoendeshwa na Vodacom Tanzania Foundation na ambao maudhui yake yamepitishwa ili kuendana na mitaala ya kitaifa kwa shule za msingi na sekondari. Jukwaa la E-Fahamu hadi sasa lina zaidi ya vitabu 80 vya kiada na zaidi ya vitabu 1,000 vya masomo ya ziada pamoja na katuni na video kadhaa za elimu.

Akiongea wakati wa kusaini mkataba, Catherine Kimambo, Mkurugenzi Mtendaji wa African Child Projects alisema, “Mlipuko wa Covid-19 ulionesha haja ya ushirikishwaji kidijitali na kuongeza kasi ya uunganishwaji kwa njia kadhaa ambazo hazikutegemewa. Hata hivyo, tofauti kati ya waliounganishwa na ambao hawajaunganishwa imeongezeka, kwani waliokuwa wanapata mawasiliano ya intaneti ya kasi waliweza kuendelea na masomo na shughuli za kikazi wakiwa mbali, wakati wale wasiokuwa na mawasiliano hayo wakiwa wameachwa nyuma. Ni nia yetu ACP kujitahidi kupunguza hali hii kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo katika sekta ya elimu.”

Mafaniko ya mradi huu yatapunguza gharama za uunganishwaji kwa mashule na wakati huo huo, kuonyesha umuhimu wa mawasiliano ya intaneti katika kuboresha mifumo ya elimu nchini na hivyo kushinkiza uwekezaji kwenye elimu ya kidijitali katika mitaala ya taifa.

Mradi huu ni mmoja kati ya shughuli kadhaa ambazo Vodacom Tanzania Plc na Vodacom Tanzania Foundation watajihusisha nazo katika jitihada zake chini ya kampeni ya Africa.Connected ambayo inalenga kuondoa tofauti katika upatikanaji wa huduma za kidijitali katika bara la Afrika. Tofauti moja kuu ikiwa ni katika upatikanaji wa elimu mtandaoni.

Wageni waalikwa katika hafla hiyo walikuwa ni pamoja na wawakilishi kutoka COSTECH, TIE, TEA, DIT, CAMARA Education Tanzania na Segal Family Foundation.

Mkurugenzi wa Asasi ya Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha sekta ya elimu kwa njia ya mtandao kupitia mpango wa School Connectivity Project utakaosaidia kuongeza ufaulu kwa asilimia 5% kwa wanafunzi nchini.


Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA, Mhandisi Samson Mwela akizungumza na waandishi wa habari kabla ya zoezi la kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha sekta ya elimu kwa njia ya mtandao kupitia mpango wa School Connectivity Project kati ya Asasi ya Vodacom Tanzania Foundation na African Child Project

Mkurugenzi wa Asasi  ya Vodacom Tanzania Foundation,  Rosalynn Mworia  (kushoto) akisaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha sekta ya elimu kwa njia ya mtandao kupitia mpango wa School Connectivity Project utakaosaidia kuongeza ufaulu kwa asilimia 5% kwa wanafunzi  nchini na Mkurugenzi wa African Child Project,  Catherine Kimambo jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia katikati ni Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA aliyemwakilisha katibu mkuu wizara ya Habari na Mawasiliano, Mhandisi Samson Mwela

Meneja Ruzuku na  Ubia (grants and partnership ) kutoka African Child Project,  Pious Sylvester akitoa mada ya namna gani Taasisi yao inatoa suluhu kwa wanafunzi kupata masomo Kidigitali kote nchini.

Mkurugenzi wa Asasi  ya Vodacom Tanzania Foundation,  Rosalynn Mworia  (kushoto) akibadilishana mkataba wa makubaliano ya kuendesha sekta ya elimu kwa njia ya mtandao kupitia mpango wa School Connectivity Project utakaosaidia kuongeza ufaulu kwa asilimia 5% kwa wanafunzi  nchini kwa Mkurugenzi wa African Child Project,  Catherine Kimambo jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia katikati ni Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA aliyemwakilisha katibu mkuu wizara ya Habari na Mawasiliano, Mhandisi Samson Mwela


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...