Na Said Mwishehe,Michuzi TV
NGOJA nikwambie kitu ndugu yangu Mtanzania kokote uliko na kwa aliye jijini la Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani na mikoa mingine iliyo karibu , ni hivi ukitaka kutembelea eneo hifadhi yoyote ile nikishauri hifadhi yako ya kwanza kuichagua iwe Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Pugu Kazimzumbwi.
Hifadhi hiyo inapatikana wilayani Kisarawe mkoani Pwani lakini kwa anayetokea Jiji la Dar es Salaam kwake inakuwa rahisi kabisa.Ndio kwanza panafika kwa urahisi kutokana na uwepo wa barabara kuu inayounganisha Pwani na Dar es Salaam.Kwa anayetokea Posta Mpya jijini Dar atatembea umbali wa kilometa kama 24 anakuwa amefika.Umeona palivyo karibu.
Najua kuna maswali ambayo utakuwa unajiuliza , na kabla ya kuendelea kueleza ngona niseme kitu, kwa mfano unaweza kujiuliza jina la Pugu Kazimzumbwi limetoka wapi? Jibu lake ni hivi linatokana na muungano wa misitu miwili yaani Msitu wa Pugu na Msitu wa Kazimzumbwi, hivyo ukiunganisha unapata Msitu wa Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi.
Nikuombe kama hutajali, najua utatumia kati ya dakika tano hadi 12 kusoma hiki ninachokiandika kuhusu Pugu Kazimzumbwi.Unachotakiwa kuweka akili na ikabaki kama kumbukumbu yako ya kudumu ni kwamba kwenye msitu huo unapendezeshwa na vitu vingi.
Ukiwa katika msitu wa Pugu Kazimzumbwi kuna kupanda milima tena ukifanikiwa kufika kileleni unaiona Dar es Salaam yoote kama ilivyo.Raha kweli asikwambie mtu.Nenda utaona utaniambia.Pia kuna uoto wa asili ambao umetanda kila kona,ukifika ndani ya msitu huo macho yako itabidi yawe 'bize' kwenye kuangalia,najua hutachoka kutazama yaliyomo , kuna ndege , wanyama wadogo wadogo, kuna chanzo cha maji ambalo bwawa lake limekuwa maarufu sana kwa watalii kuvua samaki.
Msitu wa Pugu Kazimzimbwi mzuri sana, unavutia, unapendeza lakini ukiondoa utalii uliomo humo kwa wale wenye kuamini Mizimu basi huko nako upo.Kuna mzitu unaitwa Mavoga, ni mzimu wa wenyeji wa Kisarawe, ni mzimu wa Wazaramo.Wenye kuamini wanakwenda kwenye pango la Mzimu wa Mavoga wanapiga goti, wanaomba wanatoa sadaka na ukiwasikiliza wanakwambia kabisa wamefanikiwa.
Ni uamuzi wako kuingia kwenye pango la Mavoga kwa ajili ya kwenda kuondoa mikosi au unakwenda kupata historia ya mzimu huo.Hiyo itakuwa juu yako ila utambue mzimu nao upo.Hata hivyo waongoza watalii wanayo ya kusema kabla ya kuingia kwenye himaya ya mzimu wa Mavoga.Mosi lazima muongoza watalii akaombe kibali maalumu kwa mzimu na akikubaliwa utaingia, akikataa itabidi uelezwe kwa mbali.Ukilewa hutakiwi kwenda, ukiwa na janaba pia hutakiwi.Mzimu unataka watalii wasafi.Usicheke ndio mambo ya mzimu Mavoga hayo.
Wenyewe wanasema eneo hilo lina nyoka mkubwa wa ajabu na ndio mzimu wenyewe huyo, lakini mzimu huo unatabia ya kubadilika kuna wakati unaweza kukuta amejibadili na kuwa bonge la nyoka.Uzuri wake hana shida anapenda watalii na watalii wanampenda, basi maisha yanaendelea.Ukuruhusiwa kuingia hutamuona, lakini ukienda bila ruhusa utamuona, na lazima utakimbia tu.Ndio.Unaambiwa ni bonge la nyokaaaa.
Ukiondoa mzimu wa Mavoga na utalii mwingine ambao nimekueleza , ukweli ndani ya msitu huo kuna utulivu wa kutosha, na kwa kutambua utulivu uliopo baadhi ya watalii wametengewa eneo maalum kwa ajili ya kufanya maombi, kuna eneo la kuzungumza mambo ya siri na yemekaa kitalii talii tu.
Natamani baada ya kumaliza kusoma maelezo haya uchukue uamuzi wa kwenda kutalii kwenye hifadhi hiyo na kiingili chake ni Sh.2000, hakuna gharama na kiasi hicho kinatosha kuzunguka kila kona , unachotakiwa kukifanya ni kuandaa nguvu tu ya kutosha kwa ajili ya kuzunguka.Binafsi nimwekwenda na naomba wewe nawe uende, hutajutia , hutapoteza muda wako.Fullu rahaa.
Wakati naendelea kujimwaga na kueleza kuhusu Msitu wa Pugukazimzumbwi nikung'ate sikio kidogo kwa kukumbusha kwamba msitu huo ulipewa jina la hifadhi tangu mwaka 1947 na ilipofika mwaka 2020 ulipanda hadhi na kuwa msitu wa mazingira asilia.Hapo zamani ulifahamika Msitu wa Mogo yaani Nyundo jina lenye asili ya Kigiriki na Kilatini na jina hilo lilibadilika na kuwa Pugu Kazimzumbwi baada ya nchi yetu kupata Uhuru. Ujue nataka nikwambie nini?
Nimekumbuka mtu wangu, msitu huu kwa muda mrefu licha ya uwepo wake bado haukuwa maarufu kiasi cha kutambuliwa na watu wengi.Lakini katika kipindi cha miaka minne iliyopita msitu wa Pugu Kazimzumbwi umekuwa maarufu, tena maarufu haswaa.Ni Jokate Mwegelo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kuamua kuutangaza msitu huo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Wenye kumbukumbu wanakumbuka ile wiki ya Ushoroba wa Kisarawe , kampeni iliyoanzishwa na Jokate Mwegelo kuutangza utalii uliopo wilayani humo na akajikita katika kuutangaza msitu huo.Ndio wakati tukafahamu kumbe kwenye Msitu wa Pugu Kazimzumbwi kuna Panzi mwenye rangi ya bendera ya Taifa.
Yaani kwenye huo msitu Panzi huyo anaonekana kwa urahisi na kwa ukaribu zaidi.Nenda utaona, kwanini nikudanganye!Ukienda utaona kwa macho yako.Kwani Ushoroba nini? Hili nalo ni swali ambalo unaweza kutaka kulifahamu, kwa lugha rahisi Ushoroba ni njia ya mapito ya wanyama.Kisarawe walitumia neno hilo katika kuutangaza utalii kwasababu Kisarawe nia ya kwenda Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.
Baada ya Ushoroba wa Kisarawe kuanzia hapo utalii kwenye msitu ukaongezeka, watu wakaifahamu hifadhi hiyo.Yote kwa yote ndani ya msitu huo kuna raha sana.Pamoja na yote nitoe pongezi kwa TFS Kanda ya Mashariki na Pwani inayoongozwa na Mama Calorine Malundo.
Wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya msitu huo,hakuna ambako unataka kwenda ukashinda, njia zinapita, kuna viti vimewekwa kwa ajili ya kupumzika katika eneo ambalo wanaona kabisa kwa vyovyote vile mtalii akifika hapo atataka kukaa kidogo kwa ajili ya kutafuta nguvu ya kuendelea na safari.
Nilitaka kusahau ndani ya msitu huo kuna eneo ambalo limesheheni miti aina ya mianzi (bamboo) ambayo iko pembeni kidogo mwa bwawa na cha kushangaza mianzi hiyo ina miba na inasemekana mianzi hiyo ilipandwa mwaka 1977 kwa lengo la kuzuia mmomonyoko wa udongo, lakini ni kwa wakati huo.Eneo hili ubaridi wake ni kama vile umewasha AC na kuweka nyuzi joto 12 hivi au 14.
Kuna baridi wewe, ukifika utaona na utanikumbuka.Siku za karibuni TFS -Kanda ya Mashariki na Pwani iliandaa ziara kwa wadau mbalimbali na miongoni mwa wadau hao walikuwemo waandishi wa habari.Mungu anapenzi yake nami nikawa miongoni mwa waandishi hao.
Kwani huu ujasiri wa kukuelezea nautoa wapi?Nimefika, nimezunguka, nimeona , nimefurahi na kubwa zaidi nime -Enjoy .Kuzuri sana , ujue kwenye msitu huo kuna eneo la mapango ya Popo, ukiingia unawakuta kibao wamejazana kama kumbikumbi, halafu unaambiwa popo hao wanalala Kazimzumbwi na wanaenda kutafuta chakula Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Utaniuliza kwanini, hata mimi sijui, sijauliza ila siku ukipata nafasi ya kwenda usiache kuuliza.Nakuamini ujue.Basi bwana kwenye ile ziara ya wadau wa utalii wakiwemo waandishi wa habari, Mhifadhi wa Misitu kupitia Wakala Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kisarawe Fred Ndandika anasema kutoka ndani na nje ya nchi wameongezeka na asilimia 70 ni watalii wa ndani."Msitu huu una mazingira asilia na tunatoa huduma ya utalii Ikolojia , kuna vivutio vingi , karibu uje uone."
Kwa upande wake Mongoza watalii Omary Zebo aliyekuwa na jukumu la kututembeza ndani ya msitu huo ukiondoa utalii wa aina mbalimbali , kuna utalii wa wanyama wadogo wadogo wakiwemo Komba na Ngedere.
Wakati Shaban Feruz Kiula ambaye ni Ofisa Misitu Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki yenye mikoa mitatu ya Dar es Salaam ,Pwani na Morogoro , anasema "katika kanda yetu tuna vivutio mbalimbali , kwa mkoa wa Pwani tuna vivutio katika hifadhi ya Msitu wa Mazingira ASilia Pugu Kazimzumbwi yenye safu tatu ya Pugu , safu ya Pugu ,safu ya Kazimzumbwi na safu ya Vikindu.
"TFS pia tunasimamia kivuto kilichopo Rufiji kule kuna Chemchem Maji ya Moto, ambapo huko unakuta maji yanachemka pasiko kuwa na moto na tunavyo vivuto vya mambo ya Kale kwenye Mji wa Bagamoyo pamoja na Magofu ya Kaole.Pia tunasimamia Msitu wa Mazingira Asilia Uzigua.
"Tukienda Morogoro tuna Uruguru pamoja na Mkingu, hiyo yote inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Kanda ya Mashariki.Leo(siku tuliyokwenda) tukiwa na waandishi wa habari kwa kutambua nafasi yao katika jamii yetu hasa ya kutangaza utalii.Katika msitu wa Pugu Kazimzumbwi kuna utalii wa kila aina, nitumie nafasi hii kuwaomba Watanzania na wasio watanzania waje kufanya utalii kwenye msitu wetu huu mzuri."
Sasa nihitimiishe kwa kuelezea umuhimu wa msitu huo kwa maisha ya binadamu na hasa wanaoishi Dar es Salaam.Msitu wa Hifadhi ya Mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi ndio mapafu ya Jiji la Dar es Salaam.Ndio msimu ambao hewa safi ambayu inavutwa na kila mmoja wetu inatoka kwenye msitu huo ndio kisa ya kuwa mapafu ya Dar es Salaam.
Hivyo ukishindwa kwenda kuandalia utalii uliopo basi kaangalie hata Mapafu ya Jiji la Dar es Salaam.Ukiufuatilia vizuri msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni kama vile Mungu ameupendelea ingawa tunajua Mungu hana upendeleo.
Alamsiki, Tuwasiliane 0713833822
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...