Adeladius Makwega-DODOMA

Katika matini ya iliyotangulia nilikuelezea juu ya asili ya Warufiji, nilielezea koo mbalimbali za kabila hili na asili yake kutoka kwa Wahehe, Wamatumbi na Wanyagatwa.

Mara baada ya kutoka matini ya kwanza nilipata maswali kadhaa kutoka kwa Wandenge (Wandengereko) ambao ni mabingwa wa kuupepeta mdomo. Ndugu hawa waliniuliza juu majina ya koo zao, ati mbona hayamo katika orodha niliyoitoa?

Jibu katika hili ni moja tu, katika majina mengi ambayo yanatumiwa sana na makabila mengi kwa sasa ni majina ya utani ambayo walipewa baadhi ya ndugu zetu kwa sababu mbalimbali.

Mathalani Jina MA-KWEG-A linatokana na neno la kibantu KWEGA likimaanisha kuvuta kitu/kumvuta mtu.

Juma ni mkwegaji wa watu katika ulozi

Akimaanisha kuwa ndugu Juma ni mshawishi wa watu katika ulozi.

Ndiyo maana Wapogoro, Wamatumbi, Wanyamwezi na makabila kadhaa wanalitumia jina hilo. Kwa hiyo yapo majina kama hayo mengi ambayo yanatokana na kazi anayoifanya mtu au sifa yake.

Kwa hiyo ndugu yangu MWAGARA na Warufiji wote akiwamo Sudi Mnete hata kama majina yenu hayamo katika katika orodha yangu nakupa kazi tu ya kuuliza maana ya jina hilo utabaini kuwa jina lako lina maana.

Kitendo cha koo mbalimbali zenye asili za makabila hayo kuoleana kilijenga udugu baina yao na jambo hilo lilisadia sana kujenga utani baina ya koo na koo. Wakati wa kuoa kwa Warufiji bwana harusi na ukoo wake walifunga safari ndefu ya kumfuata bibi harusi na walipofika huko waliposa na kurudi naye.

Kitendo cha ukoo mmoja kuoana na ukoo mwingine kilijenga udugu na utani baina yao. Huku ukoo uliomtoa bibi harusi ukijiona wenyewe kuwa bora ya mwezake. Huku ukoo wa bwana harusi na wenyewe ukijinasibu kuwa wamemposa bibi harusi wa ukoo mwingine.

Kama unavyofahamu Wandengereko ni wazungumzaji sana wenye maneno mengi mno, kujinasibu ni miongoni mwa utamaduni wao. Ndugu hawa ni watu wa maneno tu si watu wa kupenda fujo, kwani hata historia yao inaonesha kuwa hata kabila lenyewe liliibuka baada ya vita kadhaa kwisha watu wakawa na amani.

Kwa Warufiji, kuoana ni ruhusa bila ya kipingamizi, kwa mtu ambaye ni mtani na mtani mwenzake na hata kwa kabila ambalo si watani kwani hilo linasababisha kujenga udugu ambao haukuwepo hapo awali.

Katika kutaniana huwa ni mwiko kupigana au kuuana kwani hayo hayamo katika utani. Ifahamike wazi kuwa Warufiji hawakuwa watu wa ugomvi na kukorofishana na makabila jirani kama kulikuwa na ugimvi ulikuwa wa koo zile za Kingoni, Kihehe na Kimatumbi kutoka katika mapigano awali kabla ya kuhamia jirani na Mto Rufiji.

Kwa mfano Warufiji walikuwa wakitaniana kwa kupokonyana mali kama mashamba awe mtani wako, akifanya hivyo na mwenye mali hiyo kama akigoma basi mhusika huyo iliaminika atapatwa na ukoma na ukoma huo hauwezi kumuacha hadi kufa.

“Jambo hilo lilifanya wengi wao waliogopa mno kuupata ukoma huo kwa hiyo mtani aliweza kuchukua mali atakavyo na kulima shamba hilo ambapo baadaye aliweza kulirudisha.”

Anasema H Ngayonga katika maandishi yake ya UTANI RELATIONSHIP: THE RUFIJI.

Kabila hili pia linaamini mno katika uchawi. Kwa imani ya Warufiji mchawi ni mtu mbaya sana na uchawi maana yake ni uadui. Kwa hiyo mtu ambaye anafanya utani na mwezake hawezi kumfanyia uchawi, hapa mtani huwa ni ndugu na si adui.

Kipi kitaendelea?


Subiri matini ijayo.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...