Na Faraja Mpina na Chedaiwe Msuya, WHMTH, DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amelikumbusha Jeshi la Polisi Tanzania kuwa linalo wajibu wa kujifunza na kuwaelimisha wengine kuhusu makosa ya mtandao, namna ya kujilinda na kuchukua tahadhari dhidi ya makosa ya mtandao
Dkt. Yonazi ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya usalama mtandao kwa Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa, Wakuu wa Vikosi na Wakuu wa madawati ya Upelelezi wa Jeshi la Polisi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar yanayofanyika kwa siku tano jijini Dodoma kuanzia tarehe 21 Machi hadi tarehe 25 Machi, mwaka 2022
Amesema kuwa, Jeshi la Polisi linalo wajibu wa kujifunza kila siku, kwa kuwa wao pia ni washirika katika ulimwengu wa mtandao kupitia matumizi ya simu janja lakini pia Wimbo wa Jeshi la Polisi unasema wazi kuwa wana jukumu la kulinda usalama na haki za wananchi ambapo utekelezaji wa jukumu hilo unafanyika katika ulimwengu mpya wa kidijitali
“Dunia inabadilika kuna uhalifu mwingi unaofanyika kwa njia ya mtandao na watu wa makundi yote kwa kukusudia au bila kukusudia, hivyo watendaji mnapopatiwa elimu mna wajibu wa kuelimisha wengine kupitia nafasi za utendaji mlizo nazo sasa”, Amezungumza Dkt. Yonazi
Ameongeza kuwa, “Ukimchapa mtoto lazima umfahamishe kwanini umemchapa na kosa ni lipi, vivyo hivyo kwenye makosa ya mtandao, kabla ya kuyashughulikia ni vema wananchi wapatiwe elimu na kufahamu makosa ya mtandao ni yapi”.
Dkt. Yonazi ameyazungumzia mafunzo hayo kuwa yanatoa taswira nzima na uelekeo wa nchi katika kushughulikia masuala ya usalama mtandao ili kufikia malengo yanayotarajiwa huku wajibu wa Wizara hiyo ni kuhakikisha mafunzo hayo ni endelevu na usalama katika mtandao unasimamiwa vizuri
Akizungumza na hadhira hiyo Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI) CP Camilius Wambura ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa kuwa yatawasaidia watendaji wa Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza ujuzi utakaowafungua zaidi na kupanua wigo wa kupambana na uhalifu hasa wa makosa mtandao
“Teknolojia inabadilika kila kukicha hivyo mafunzo ya mara kwa mara kwa watendaji wetu yanahitajika ili kuendana na kasi ya mabadiliko haya kwa watendaji kupitishwa wapi tulipo na wapi tunaelekea katika kukabiliana na uhalifu wa mtandao”. Amezungumza Wambura
Naye Mkaribu Mwandamizi wa Polisi, SSP Joshua Mwangasa ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuwajengea uwezo watendaji wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na hatua zinazoendelea za kuanza ujenzi wa maabara za uchunguzi wa kisayansi zitakazojengwa kikanda katika mikoa sita ya Mbeya, Arusha Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar ambazo zitasaidia kupanua wigo wa uchunguzi wa makosa ya mtandao.
Mafunzo hayo ya usalama mtandao yanatolewa kwa watendaji wapatao 100 wa Jeshi la Polisi Tanzania ikiwa ni muendelezo wa mafunzo yaliyotolewa mwezi Februari mwaka huu kwa watendaji wengine wa Jeshi hilo na sasa ni zamu ya wasimamizi wao ambao ni Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa, Wakuu wa Vikosi kama vile TAZARA na Bandari, Wakuu wa Madawati ya Upelelezi wa Mikoa na Wakufunzi wa vyuo vya Polisi nchini.
Home
HABARI
DKT. YONAZI ALIKUMBUSHA JESHI LA POLISI WAJIBU WA KUJIFUNZA NA KUTOA ELIMU YA USALAMA MTANDAO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...