Na.WAF-Ruvuma
Wananchi wameaswa kulinda afya zao za Kinywa na meno kwa kufuata njia sahii za kujikinga
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani Ruvuma.
Prof. Makubi amesema swala la kujikinga na Magonjwa ya Kinywa na Meno ni muhimu zaidi kuliko kusubiri kuingia kwenye hatua ya matibabu.
"Usafishaji wa kinywa kwa usahihi, matumizi ya miswaki yenye sifa stahiki, na udhibiti wa ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kufanya uchunguzi wa Kinywa na Meno walau mara moja kwa mwaka ni miongoni mwa mambo ya msingi na ya lazima ili kuwa na Kinywa chenye Afya njema" Amesema Prof Makubi .
Aidha, amesema matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku pamoja na unywaji wa pombe uliopitiliza huchangia kupata madhara ya magonjwa ya fizi, saratani kwenye ulimi, mdomoni na koo.
Hata hivyo Prof. Makubi amewahimiza wananchi Kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kuweza kupata huduma kwa gharama nafuu na haraka.
"Wito wangu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na taifa nzima tuendelee kujitokeza kwa hiari kujiunga na mfuko wetu wa bima ambao utasaidia kuboresha huduma zetu na kupata huduma bora " Amesema Prof. Makubi
Prof. Makubi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha huduma ya Kinywa na Meno zinaimarika, kwa kuendelea kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha miundombinu ya matibabu hayo katika hospitali na vituo vya afya.
"Takwimu zinaonyesha jumla ya Wagonjwa 685,224 walihudhuria kwa ajili ya matibabu ya Kinywa na Meno katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya kwa mwaka 2021, Wagonjwa 506,950 (74%) walikuwa na tatizo la kutoboka kwa meno ilihali watu 69,318 walikuwa na Magonjwa ya Fizi."
Kwa upande mwingine Prof. Makubi amemshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za afya zina imarika kwa kuendelea kununua vifaa vya kisasa, kujenga miundombinu na kuboresha matibabu kwa ujumla.
"Kwenye fedha za Uviko - 19 uwekezaji mkubwa umefanyika katika vituo vyetu vya afya kwa kujenga vyumba vya kutibu wagonjwa mahututi na dharura pamoja na vifaa vya kisasa" Amesema Prof Makubi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...