Na Maelezo Zanzibar 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ameridhia kubadilishwa matumizi ya jengo lililokuwa “Ikulu ndogo ya Kibweni” na sasa jengo hilo litatumika kama kivutio kipya cha watalii nchini.

Aidha jengo hilo kwa sasa litajulika kwa jina la “Makumbusho ya Kasri ya Kibweni”.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Simai Mohamed Said ameyasema hayo katika uzinduzi wa Makumbusho hiyo mpya, hafla iliyofanyika hapo kibweni mjini Zanzibar.

Amesema hatua ya Rais kuridhia kubadilishwa matumizi ya jengo hilo ni miongoni mwa juhudi zinazofanywa na Wizara yake ya kubuni vyanzo vipya vya utalii na kuongeza mapato nchini.

Akielezea kuhusu historia ya Kasri hiyo, Waziri Simai alisema ilijengwa mwaka 1915 na Sayyid Khalifa bin Haroub aliyetawala Zanzibar mwaka 1911 hadi 1960. Kwa wakati huo Kasri hilo lilijulikana kwa jina la “Kasru Saada” ikiwa na maana “nyumba ya starehe”.

Amesema Msanifu wa majengo wa Serikali maarufu wakati huo Bw. John H. Sinclair ndiye aliyesarifu ujenzi wa jengo hilo katika mtindo wa kiislam.

Waziri Simai amefahamisha kuwa, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, Jengo hilo lilikuwa chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar likijulikana kama Ikulu ndogo ya Kibweni. Kasri hilo lilitumika kama sehemu ya mapumziko kwa Marais wa awamu tofauti pamoja na kufanyia mikutano ya kiserikali.

Waziri huyo aliwaomba Watendaji wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale kuhakikisha wanalitumia vyema jengo hilo ili kukidhi matakwa yaliyokusudiwa.

Amewataka wafanyakazi watakaohusika kulitangaza vyema Jengo hilo kwa wageni na wenyeji ili walitembelee na kujua historia yake kwa undani.

“Nashauri wageni wataokuja kutembelea Kasri hili tusiwatoze Tozo kubwa, tuwatoze tozo inayoendana na hali halisi ili washawishike wengi kuja hapa, ni vyema pia katika ndani ya Kasri kuwepo kwa Mgahawa ili kuvutia zaidi wateja” alishauri Waziri Simai.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Fatma Mabrouk amewaomba wadau na Makampuni ya kutembeza wageni kuwapeleka wageni hao katika Makumbusho ya Kibweni kujionea historia yake.

Akitoa nasaha zake katika hafla hiyo Balozi mdogo wa China, Zanzibar Shang Shisceng amesema China itaendelea kutoa msaada wa kitaam kwa Zanzibar ikiwepo kuwapatia mafunzo ya Mapishi wafanyakazi wa Mahoteli Zanzibar ili kuwavutia watalii wanaotokea mashariki ya mbali ikiwemo China.

Jengo hilo ambalo kwa sasa linatumika kama kivutio kipya cha Utalii ndani yake kuna maonesho yanayoelezea maisha na matumizi ya jengo hilo tokea wakati lilipojengwa hadi sasa. 


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...