NA BALTAZAR MASHAKA,Ilemela


OFISA Elimu (sekondari) wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Emmanuel Malima,amezindua ujenzi wa bweni la hosteli ya wasichana katika Shule ya Sekondari Kilimani,ukiwa mkakati wa kukabiliana na mimba za utotoni,utoro kwa wanafunzi wa kike na kuongeza ufaulu wao.

Akizindua ujenzi huo wa msingi wa bweni jana kasha akaendesha harambee ya ujenzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala,Malima,alisema mradi huo umebuniwa na wananchi wenyewe kutokana na mahitaji ya watoto kupata muda wa kujifunza na kujisomea.

Alisema wananchi na jamii wamejitolea nguvu zao, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri pia wamejitoa kuhakikisha watoto wa kike wanapata muda wa kujifunza na kujisomea kwenye mazingira mazuri yenye utulivu yatakayosaidia walimu kukuza taaluma na kuongeza ufaulu wa watoto.

Malima alieleza mahitaji ya mabweni kwenye shule za sekondari ni makubwa na mkakati wa idara ya elimu na halmashauri ni kuhamasisha jamii na wananchi kuchangia miundombinu hiyo ili kupata matokeo chanya kwenye shule za Halmashauri ya Ilemela.

Alisema bweni hilo likikamilika watoto watasoma vizuri zaidi tofauti wakitokea nyumbani ambapo aliendesha harambee ya ujenzi wa msingi wa bweni hilo na kuchangia sh. milioni 1 kwa niaba ya idara ya elimu Manispaa ya Ilemela.

Mmoja wa wadau wa shule hiyo Mhandisi Mnandi Mnandi,alisema kauli mbiu ya Kilimani ni kutokomeza sifuri na daraja la nne,hivyo alichangia sh. 350,000 na kuahidi kununua viti vya walimu na akawataka wazazi kujitathmini na kuchangia elimu ya watoto wao.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela,Nelson Mesha alisema ndicho chenye ilani inayotekelezwa,lazima kione mafanikio kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu na taaluma, lengo sekta ya elimu ipige hatua kubwa.


“Suala la elimu Ilemela imebadilika,Rais Samia Suluhu Hassan ametupunguzia mzigo mkubwa na shule hizi ni zetu kwa faida ya watoto wetu na vizazi vyetu,wananchi tunaposhirikishwa kwenye miradi hii tuhamasike,hakuna mjomba kutujengea mabweni na madarasa,”alisema Mesha.

Alichangia mifuko 10 ya saruji na kuwapongeza walimu,ofisa elimu na halmashauri kwa kusimamia elimu kwa weledi hali inayowawezesha walimu kuwaandaa watoto kuwa watalaamu wa baadaye.


Awali Mkuu wa Shule ya Kilimani,Gerana Majaliwa,alisema mpango wa hosteli ya watoto wa kike uliridhiwa na wazazi,hivyo ujenzi wa msingi wa bweni hilo litakalokuwa na vyumba 20,matundu 6 ya vyoo yakiwemo mawili ya wenye mahitaji maalumu na sehemu ya kufungulia nguo utagharimu sh. milioni 31.6.

Alisema bweni hilo litachukua wanafunzi zaidi ya 150 na kutokana na mafanikio ya kitaaluma kwa wasichana wanaokaa shuleni ambapo ufaulu wao umeongezeka,nidhamu imeimarika,kupungua kwa idadi ya wanaopata ujauzito,changamoto ya utoro,kuchelewa shuleni sababu ya umbali na usafiri imepungua.

“Mradi wa hosteli ulianza mwaka 2020 ukilenga kupunguza utoro na mimba kwa watoto wa kike ili kuwapa fursa ya kutimiza ndoto zao,kwenye harambee sh.milioni 1.069 taslimu zilikusanywa,ahadi ya fedha sh.milioni 1.6 na mifuko 70 ya saruji,”alisema Majaliwa.

Aidha shule ina changamoto ya ukosefu wa bwalo la chakula na jiko,uzio,matundu ya vyoo na viti vya walimu ambapo mfadhili The Desk & Chair Foundation amejitolea kujenga matundu 20 na uongozi unasubiri kusaini mkataba mradi huo uanze.

Alieleza kuwa uongozi wa Kilimani Sekondari unampongeza Rais Samia kwa kuthamini elimu na kuipatia sh.milioni 40 za vya vyumba viwili vya madarasa na samani (viti na meza),pia Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala kwa kuridhia kuzindua ujenzi wa msingi wa hosteli ya wasichana.

“Kipekee tunawashukuru mkuu wa wilaya kwa kupambana na kusaidia kutatua changamoto ya maji shuleni,Mbunge wa Ilemela, Dkt.Angeline Mabula na Mkurugenzi wa Manispaa,Mhandisi Modest Apolinary,Chama Cha Mapinduzi kwa michango na maelekeo mazuri,wajumbe wa bodi,walimu,wazazi na wanafunzi,”alisema Majaliwa.

Baadhi ya wanafunzi wa hosteli,Getruderose Joseph wa kidato cha nne na Nuryat Mohamed wa kidato cha kwanza,walisema kuishi hosteli ni tofauti na nyumbani,kumewaongezea ari ya kujifunza zaidi sababu ya madhari na mazingira tulivu ya kujifunzia.






Baadhi ya wananchi na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kilimani,wakitoka kwenye uzinduzi wa ujenzi wa bweni la hosteli ya wasichana wa shule hiyo jana ili kukabiliana na mimba na utoro.Picha zote na Baltazar Mashaka.

Emmanuel Malima ambaye ni Ofisa Elimu Sekondari,akishiriki ujenzi wa bweni la hosteli ya wasichana Kilimani sekondari baada ya kuuzindua jana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...