Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kumekuwepo na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya mawasiliano nchini katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Nape amesema hayo leo Machi 14,2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya mwaka mmoja wa Wizara hiyo katika Serikali ya Awamu ya Sita ambapo ameeleza uwekezaji katika sekta hiyo umegawanyika katika maeneo makubwa matatu , uwekezaji sekta binafsi, uwekezaji wa Serikali na uwekezaji wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kwa pamoja.

Amesema takwimu zinaonesha ukuaji wa sekta hiyo katika kipindi hicho kati ya Machi 2021 hadi Februari 2022 laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka 51,210,914 hadi 55,396,190 sawa na ongezeko la asilimia 8.2.Idadi ya akaunti za pesa kupitia simu za mkononi imeongezeka kutoka 27,326,938 hadi 32,720,180 sawa na ongezeko la asilimia 19.7.

Amesema idadi ya watumiaji wa huduma za intaneti imeongezeka kutoka milioni 28 Machi mwaka 2021 hadi milioni 30 Februari 2022 ambalo ni ongezeko la asilimia 7.1.Watoa huduma na huduma ziada wamefikia 102 ikilinganishwa na 66 Machi 2021 sawa na asilimia 54.5.Pia bei ya mwingiliano kati ya watoa huduma imeshuka kutoka Sh.2.6 kwa dakika mwaka 2021 hadi Sh.2.0 kwa dakika mwaka 2022, ambalo ni punguzo la asilimia 23.1.

"Kwa upande wa Serikali zaidi ya Sh.bilioni 93 zimetumika kuwekezwa kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya mawasiliano .Baadhi ya shughuli zilizofanyika ni kukamilisha ujenzi wa minara 12 maeneo ya mipakani na kanda maalum, kupeleka huduma za mawasiliano katika hifadhi ya Burigi-Chato na maeneo mengine jirani.

"Kupeleka huduma ya mawasiliano kwenye ofisi 10 mpya za halmashauri za Wilaya, ujenzi wa minara 42 ya mawasiliano kwa Zanzibar, kuongeza uwezo wa minara 127 nchini kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili kuongeza kasi ya intaneti kwenye maeneo hayo.Aidha ujenzi wa kilometa 72 za mkongo wa Taifa na kuwezesha maunganisho ya mkongo kwa nchi ya Msumbiji kwenye eneo la Mtambaswala.

"Na kukamilisha upembuzi yakinifu wa kujenga mkongo wa mawasiliano kuunganisha nchi ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo(DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.Kwa mwaka 2021/2022 Serikali imetenga Sh.bilioni 170 kuwezesha kujengwa kwa mkongo wa Taifa ambapo Wizara imeingia mkataba wa mashirikiano na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)kwa ajili ya kufanya kazi pamoja ya kupitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye miundombinu ya umeme,"amesema.

Nape amesema hatua hiyo imepunguza gharama za ujenzi wa mkongo na kuharakisha mradi huo ambapo zilikuwa zijengwe kilometa 1,880 lakini kutokana na mkataba huo zitajengwa kilometa 4,442 katika Wilaya 23 nchini."Hii itapelekea ujenzi wa mkongo kufika wilaya 66 kati ya wilaya 139, kazi inayoendelea baada ya Wizara kusaini mikataba 15 inayogharimu Sh.bilioni 123."

Ameongeza katika kipindi cha mwaka mmoja Machi 2021 hadi Machi 2022 kilometa 409 zimejengwa na kufikisha kilometa 8,319 sawa na asilimia 55 ya lengo la kufikia kilometa 15,000 mwaka 2025.Pia Serikali imekamilisha ukarabati wa kilometa 105 za ujenzi wa mkongo kati ya Jiji la Arusha na Namanga kupitia miundombinu ya TANESCO.

Amefafanua hatua hiyo itaongeza ubora wa mawasiliano na mapato kutokana na maunganisho ya mkongo na nchi jirani.Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL) limewezesha jumla ya Sh.bilioni 3.7 kwa ajili ya kufikisha miundombinu ya mawasiliano katika eneo la mradi wa kufua umeme la Julius Nyerere.

Aidha Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TTCL imewezesha uungwaji katika mtandao wa intaneti na data kupitia mkono kwa vituo zaidi ya 300 vya Mahakama, halmashauri zaidi ya 169, matawi ya mabenki 600, vituo vya uongozaji ndege, vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 20, bandari zote nchini pamoja na huduma za afya kwa hospitali zote za rufaa nchini.

Pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha upanuzi wa njia za kimataifa za mawasiliano ya intaneti kutoka kiwango cha 12.7Gbps hadi 18.7Gbps sawa na ongezeko la asilimia 47.Aidha Serikali kupitia TTCL imefanikisha kuongezeka mauzo ya mkongo wa Taifa kiasi cha Dola za Marekani 11,432,204.00 kutoka Dola 79,781,776 Machi, 2021 hadi kufikia dola 91,213,980.92 sawa na ongezeko la asilimia 14.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...