WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kuboresha mazingira ya utendaji wa waandishi wa habari nchini.
Alisema toka awamu ya sita iingie madarakani iko katika hatua mbalimbali za kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira mazuri, na kuongeza kuwa mpaka sasa hawajapata kipingamizi chochote cha hayo wanayoyafanya, na hiyo ni dalili kuwa wanakwenda vizuri.
“Kikubwa we are in the right direction, ni vizuri tukaambiwa tunakwenda vipi katika kuboresha mazingira ya tasnia ya habari hapa nchini, lakini mpaka sasa hatujaambiwa kitu, hii inaonekana tunakwenda vizuri,” alisema Waziri Nape.
Waziri alisema kuwa wao kama Serikali wanajua kote walikopita kuna baadhi ya mambo wameweza kuyabadilisha na mengine yatachukua muda mrefu, hivyo aliwataka wadau wa habari kumpa muda na pia kumwamini ili afanye kazi yake.
Nape aliyasema hayo Machi 17, 2022 Jijini Dar es Salaam alipokutana na taasisi za habari ili kufahamiana na kujua shughuli za taasisi hizo.
Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni Misa-Tan, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na International Media Support (IMS).
Alisema mikutano kama hii ni mizuri kwa sababu inasaidia kutatua baadhi ya changamoto ambazo siyo lazima zitoke nje na zipigiwe kelele huko barabarani.
Waziri Nape alirudia kauli yake kuwa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ili kutatua changamoto zilizojitokeza.
Alisema hana nia ya kuvifungia vyombo vya habari lakini pia vyombo vya habari viwe makini katika utendaji kazi wake.
Alisema hata sasa hivi kuna makosa vyombo vya habari vinafanya na makosa hayo mengine yameanishwa kwenye sheria, lakini Serikali imeyanyamazia siyo kwa sababu sheria haipo ila ni kwa sababu wameamua kufanya mabadiliko, hivyo ameamua kuvinyamazia baadhi ya vipengele vya sheria hiyo.
“Baadhi ya vifungu tumevinyamazia siyo kwa sababu havipo, ila tunajua vipo, kuna Katiba, Sheria, Kanuni, lakini tukasema tutumie busara tuone inasemaje,” alisema.
Alitoa mfano wa gazeti moja (jina linahifadhiwa) ambalo liliandika habari bila kufanya utafiti wa kutosha, matokea yake gazeti likaandika habari ya uongo kuhusu kupitishwa kwa sheria, “Niliwaita nikawauliza kwa nini huyu mwandishi hakulifuatilia hili suala mpaka mwisho, lakini hakulifungia hilo gazeti na badala yake walijadiliana na kuyamaliza.
Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari akizungumza na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za habari ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jijini Dar es Salaam Machi 17,2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...