Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia vijiji 67 vilivyokuwemo maeneo ya hifadhi katika mkoa wa Morogoro kubaki ili kuwawezesha wananchi wake kuendelea na shughuli zao bila matatizo.

Hatua hiyo ya Rais Samia ni juhudi za za Serikali ya Awamu ya Sita kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

Kamati ya  Mawaziri wa Kisekta inayoongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji mapendekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji na mitaa 975.

Baadhi ya Mapendekezo hayo ni kubakisha vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi na kuhakiki pamoja na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa kwa mashamba yasiyoendelezwa.

Akizungumza na uongozi na watendaji wa mkoa wa Morogoro kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika mkoa huo mwishoni mwa wiki, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema mkoa huo unahusisha vijiji 81 kati ya 975 yenye migogoro ya matumizi ya ardhi.

‘’Katika kutafuta suluhu ya migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye mkoa huu, viijiji 67 vitabaki katika maeneo yake na vijiji/mitaa 14 vitafanyiwa tathmini’’ alisema Dkt Mabula.

Moja ya eneo lenye mgogoro wa matumizi ya ardhi mkoani Morogoro ni Bonde la Mto Kilombero linalohusisha Pori Tengefu na Hifadhi ya Misitu inayochangia maji kwenye Mto Rufiji unaotumika pia kupeleka maji kwenye mradi wa kimkakati wa Bwawa la Mwl Nyerere.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, pamoja na maamuzi hayo ya serikali kila taasisi itakuwa na jukumu la kuhakikisha inalinda maeneo yake ya ardhi ili yasiweze kuvamiwa tena na wananchi.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa maagizo kwa Watendaji wa Serikali kuhakikisha taratibu zinafuatwa katika kusimamia utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa na serikali kwa kuwa kutosimamiwa vyema kwa maamuzi hayo kumechangia kwa kiasi kikubwa uwepo migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali.

Alionya wananchi wenye tabia ya kuvamia mashamba yanayofutwa na serikali na kuzitaka mamlaka za upangaji ambazo ni halmashauri kuhakikisha maeneo hayo yanapangiwa ile mipango wa matumizi ya ardhi kabla ya kuanza kutumika.

‘’Pale ambapo serikali imefuta mashamba, mashamba hayo lazima yarudi kwenye mikono ya halmashauri ili mpango wa matumizi uweze kuandaliwa’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Merry Masanja mbali na kuwapongeza wakuu wa wilaya kwa kazi kubwa wanayoifanya katika wilaya zao alisema bado kuna changamoto katika usimamizi wa maeneo hasa yale ya hifadhi.

‘’Kuna changamoto nyingi zinazosababishwa na watendaji wa serikali hasa katika maeneo ya hifadhi hapa morogoro kuna vijiji 46 vimesajiliwa ndani ya maeneo ya hifadhi’’ alisema Merry Masanja.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Hamis Chillo alieleza umuhimu wa kutolewa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala ya hifadhi na kusisitiza kuwa busara lazima itumike katika kutekeleza maamuzi yanayotolewa na serikali.

‘’Watu wanahitaji kupata elimu ya uhifadhi na wakiipata taaluma katika masuala hayo basi utekelezaji maamuzi ya serikali itakuwa rahisi kutekelezwa, busara lazima itumike’’ alisema Chillo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa mkoa wa Morogoro wakati wa ziara ya Mawaziri wa Kisekta kupeleka mrejesho wa Uamuzi wa Baraza la Mawaziri juu ya utatuzi wa wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 26 Machi 2022.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Merry Masanja akizungumza katika kikao baina ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta na uongozi wa mkoa wa Morogoro wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutoa Mrejesho wa Uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 26 Machi 2022.  .

 Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikunte akichangia hoja kwenye kikao baina ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta na uongozi wa mkoa wa Morogoro wakati wa ziara ya Kamati kupeleka mrejesho wa Uamuzi wa Baraza la Mawaziri juu ya utatuzi wa wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 26 Machi 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...