Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kwa dhati kuondoa uzembe na vitendo vyovyote vya rushwa mahali pa kazi hii ikiwa ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mkutano wa sita wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambao ulipitia makadirio ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Prof. Janabi alisema ni wajibu wa kila mfanyakazi kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahali pa kazi,anafanya kazi kwa bidii, anatekeleza malengo aliyopangiwa katika muda uliopangwa. Vilevile kwa mfanyakazi anatakiwa kutunza mali na vifaa alivyokabidhiwa kufanyiwa kazi na kuwahi kazini ili kuiwezesha Hospitali hiyo kusonga mbele katika kutekeleza malengo ya Serikali pamoja na kutoa huduma a bora kwa wananchi.
“Mfanyakazi wa JKCI anatakiwa kufahamu ni huduma ya kiwango gani aitoe kwa wagonjwa na ndugu zao wakati huo huo ni lazima ajue bajeti iliyotengwa kwa ajili ya shughuli zake ndani ya Taasisi ili afanye kazi kwa kuzingatia malengo na rasilimali zilizokadiriwa kutumika”,.
“Utaratibu ambao bajeti huandaliwa kulingana na mipango kazi iliyoainishwa kwenye mpango mkakati wa Taasisi kulingana na vyanzo vya mapato na rasilimali zilizopo. Mtindo huu wa bajeti huonesha wazi wazi utendaji wa kila idara hususan kwa mtu mmoja mmoja kulingana na vipimo vya utendaji wake”, alisema Prof. Janabi.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mkurugenzi wa Fedha na Utawala CPA Agnes Kuhenga alisema bajeti hiyo ya shilingi bilioni 44.6 imelenga zaidi katika ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi, madawa, ujenzi wa jengo la utawala na vipimo, mafunzo kwa watumishi na mishahara na posho za wafanyakazi.
Aidha CPA Agnes alisema katika kuboresha kipato cha wafanyakazi, Taasisi hiyo ilianzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) mwaka 2019 ambayo hadi sasa kina wanachama 91 ambao ni wafanyakazi wa JKCI na tayari kimeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 200.
“Kuwepo kwa JKCI SACCOS kumewasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyakazi wetu kuweka akiba na kupata mikopo ambayo wanaitumia katika shughuli za maendeleo yao binafsi ili kujikwamua kiuchumi. Jambo la kufurahisha ni kuwa wanachama hawa wanalipa mikopo yao kwa wakati na hivyo kuiwezesha SACCOS hii kuwa na mafanikio makubwa zaidi”, alisema CPA Kuhenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Prof. William Mahalu aliipongeza managenenti ya JKCI kwa kuwa na maelewano mazuri baina yao na wafanyakazi, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE)na baraza la wafanyakazi jambo linalosaidia kuwepo na utoaji mzuri wa huduma kwa wagonjwa na wananchi wanaowahudumia.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Kanda Bugando aliwapongeza wafanyakazi wa JKCI kwa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo wanazozitoa kwa wagonjwa na kuwaomba waendelee na moyo huo huo ili huduma hizo ziwe endelevu ili wagonjwa waendelee kutibiwa hapahapa nchini na siyo nje ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Ninawapongeza kwa bajeti nzuri mliyoiandaa ambayo imegusa idara zote za Taasisi ikiwepo kutengwa kwa fedha za kuwasomesha wafanyakazi. Ninawaomba wale ambao mtapata nafasi ya kwenda kusoma muitumie vizuri nafasi hiyo ili mtakapomaliza mrudi na ujuzi ambao utaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi”, alisema Prof. Mahalu.
Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la JKCI wakati wa kikao cha sita cha baraza hilo kilichafanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vivian Mlawi akijibu swali kuhusu mafunzo ya kutoa huduma ya kwanza kwa watumishi wakati wa kikao cha sita cha baraza la wafanyakazi kilichafanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akijibu swali kuhusu uimarishwaji wa miundombinu iliyopo katika chumba cha upasuaji mdogo wa moyo (Cathlab) wakati wa kikao cha sita cha baraza la wafanyakazi kilichafanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Ugavi na Ununuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Leah Komba akichangia mada kuhusu mafunzo ya watumishi wa Taasisi hiyo wakati wa kikao cha sita cha baraza la wafanyakazi kilichafanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa Dkt. Janeth Madete akichangia mada kuhusu umuhimu wa motisha wanazopatiwa watumishi wakati wa kikao cha sita cha baraza la wafanyakazi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) mkoa wa Dar es Salaam Sarah Rwezaula akichangia mada kuhusu ushirikishwaji na upatikanaji wa watumishi bora wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kikao cha sita cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo lililofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akiwapongeza wajumbe wa Baraza la wafanyakzi wa JKCI kwa jitihada wanazozifanya za kutoa huduma bora kwa wagonjwa wakati wa kikao cha sita cha baraza hilo lililofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha sita cha baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...