Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa hitimisho la mkutano wa 13 wa Baraza la Uongozi la Mkataba wa Lusaka(The 13rd Governing Council of the Lusaka Agreement) katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika jijini Livingston nchini Zambia.
“Nchi itafaidika na mkutano huo kwa sababu tumekuwa na changamoto kubwa ya mapambano dhidi ya maharamia wanaodhuru wanyama wetu na hivyo tutakomesha biashara haramu.” Mhe. Masanja amefafanua.
Amesema mkutano huo utafanyika mwezi Mei mwaka 2024 na unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 100 na utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa sababu kuna mashirika mbalimbali ambayo yanayojitokeza kuzisaidia nchi za Afrika ambazo zinapambana na ujangili wa misitu na wanyamapori.
Ameongeza kuwa kama Tanzania itafikia masharti yaliyowekwa, kitajengwa kituo cha kupambana na ujangili wa misitu na wanyamapori jijini Arusha lengo ni kudhibiti ujangili wa misitu na wanyamapori na kuhakikisha biashara haramu ya ujangili wa wanyamapori na misitu inakomeshwa.
Akiongelea kuhusu Mkataba wa Lusaka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zambia, Mhe.Hassan Simba Yahya amesema mkataba huo unajihusisha na kuzuia uuzaji, usafirishaji wa wanyamapori pamoja na mimea hivyo utasaidia katika kupambana na ujangili na uhamishaji wa wanyama na mimea ambayo iko katika hatari za kutoweka.
Amesema Tanzania imeshiriki katika mkutano wa 13 wa Baraza la Uongozi la Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika ambao maamuzi yake yatainufaisha Tanzania kama nchi mwanachama.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri Wanachama kutoka nchi za Congo, Lesotho, Liberia, Tanzania, Uganda na Zambia. Nchi zingine zilishiriki kama Waangalizi (Observers) ni Niger, Senegal, Angola, Malawi, Mozambique, Togo, Ivory Coast, Benin, Ghana, Guinea , Burkina Faso na Nigeria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...