Na Tiganya Vincent, Mahakama-Lushoto

Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)- Lushoto umeshauriwa kutumia rasilimali walizonazo ili kuanzisha mafunzo ya muda mfupi yatakayowasaidia kujiendesha kibiashara.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 16 Machi, 2022 wilayani Lushoto na Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Abdullah Mwinyi wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania ukiwemo wa ujenzi wa Daharia ya Wanachuo wa Kiume katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama.

Mwinyi alisema IJA ina hazina toka juu hadi chini katika sekta ya Sheria ambayo wanaweza kuitumia katika kufanya biashara kwa kutumia taaluma waliyo nayo.

Alisema ni jukumu la Chuo hicho kubuni mikakati ya kuendesha kozi za kuwanoa wahitimu katika Vyuo vikuu mbalimbali katika fani ya Sheria ikiwemo mbinu za kisheria (Legal tactics), mikakati ya kisheria (legal strategies), uandishi wa kisheria, kujadiliana kwa ajili ya maridhiano (negotiation), uandaaji wa sera na uendeshaji wa ushauri wa kisheria .

Mwinyi alisema wapo wataalamu wengi ambao wengine ni Wastaafu ambao wanaweza kuwasaidia kuendeleza wazo hilo na kukiwezesha Chuo hicho kupata fedha kwa ajili ya kujiendesha na nyingine kwa ajili ya kusaidia jamii inayowazunguka.

Mbunge huyo alisema wapo wadau ndani na nje ambao wako tayari kusaidia katika eneo hilo katika kutafuta fedha kwa ajili ya kujiendesha na kusaidia Taasisi nyingine.

Aliongeza wapo watu ambao wanaweza kutumia taaluma walizo nazo kuwasaidia kupitia ubia kati yao na sekta binafsi (PPP) katika kufanikisha zoezi la kutumia rasilimali za Chuo hicho kujiendesha kibishara.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mwanga Anania Tadayo amewataka Viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuendelea na jukumu la awali la uanzishwaji wake ili kuhakikisha linawaandaa Mahakimu kuwa na mfumo unaowiana katika kuamua mashauri.

Amesema hatua hiyo itasaidia Mhimili wa Mahakama kuendelea kuwa na Mahakimu wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na katika viwango vinavyofanana bila kupoteza mwelekeo.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Abdullah Mwinyi akizungumza wakati wa Kikao kati ya Wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo katika picha) pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto wakati Kamati hiyo ilipotembelea Chuo hicho leo tarehe 16 Machi, 2022 kwa ajili ya kukagua Mradi wa ujenzi wa Hosteli ya Wavulana inayojengwa chuoni hapo.

Picha ya pamoja: Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria (waliosimama na baadhi wameketi) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto), katikati ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka, wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Kazungu Khatibu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...