WANAVIKUNDI vya kuweka na kukopa Pemba wamesema kuwepo kwa vikundi hivyo umesaidia kuongeza na kukuza vipato vya wanawake katika jamii na kuwaepusha dhidi ya vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vinawakabili wanawake hao kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na wanavikukundi vya MWANZO NI BORA na TUPATE SOTE, vilivyopo Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba wakati wa ziara ya mafisa kutoka Chama cha Walemavu cha Norway (NAD), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) pamoja na Mwamvuli wa Taasisi za Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) iliyolenga la kujifunza jinsi vikundi hivyo vinafanya kazi.
Hadia Idi Khamis, katibu wa kikundi cha Mwanzo ni Bora, kutoka Shehia ya Michungwani alisema kupitia vikundi hivyo vimewawezesha wanawake wa Shehia hiyo kuimarika kiuchumi kutokana na faida wanazozipata kwa uwekaji wa hisa na ukopaji kwenye vikundi.
Alieleza kwamba katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano tangu ajiunge kwenye kikundi hicho kilichoanzishwa kwa usimamizi wa TAMWA Zanzibar kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar, amefanikiwa kujiimarisha kiuchumi katika nyanja mbalimbali.
“Kupitia ushiriki kwenye vikundi, nimenunua Cherehani mbili kwaajili ya shughuli zangu za ushonaji, lakini pia baada ya kugawana hisa nimeweza kumpeleka mdogo wangu chuoni kwaajili ya kujifunza ushonaji,” alisema Hadia Idi.
Akizungumza na wanavikundi hao, George Mukasa Mukisa, ambaye ni mshauri wa kiufundi kutoka Chama cha Walemavu cha nchini Norway (NAD), alipongeza juhudi za wanawake hao kujishirikisha katika shughuli za uchumi na kusema kwamba juhudi hizo zinasaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazowakabili wanawake.
Aidha alibainisha kwamba kupitia mafanikio ya shughuli za vikundi hivyo amejifunza mbinu bora za kuwawezesha Walemavu kujiinua kiuchumi kupitia vikundi ili nao waweze kujikwamua dhidi ya changamoto na vikwazo vinavyowakabili.
“Walemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi katika jamii, hasa hali ngumu ya maisha kutokana na kukosa mifumo sahihi ya kujisimamia kiuchumi, kupitia kwenu nimejifunza namna ambavyo tunaweza kuwasaidia walemavu kujiinua kiuchumi kupitia vikundi hivi,” alisema George.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alisema vikundi vya wanawake ambavyo vilianzishwa na chama hicho vimeleta mabadiliko chanya kwa wanawake Zanzibar kuondokana na utegemezi ambao uliwakwaza wanawake wengi kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar (WEZA), umesaidia kufanikisha kuwaamsha wanawake Zanzibar kuchangamkia fursa za kiuchumi kwa kutumia ujuzi na mbinu za kibiashara ambazo wamewezeshwa wanawake hao.
Mshauri wa kiufundi kutoka Chama cha Walemavu cha nchini Norway (NAD), George Mukasa Mukisa akizungumza na wanakikundi cha TUPATE SOTE.
Mshauri wa kiufundi kutoka Chama cha Walemavu cha nchini Norway (NAD), George Mukasa Mukisa akipokea bidhaa kutoka kwa mwanakikundi chTUPATE SOTE kilichopo kijiji cha Mavungwa, Wilaya ya Chake chake, Mkoa wa kusini Pemba wakati wa ziara yake kuangalia shughuli za kikundi hicho.
(PICHA NA TAMWA ZANZIBAR)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...