*******************
Na. WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kufikia Julai Mosi 2022 Hospitali ya Mlonganzila ianze kujitegemea yenyewe badala ya kuendelea kuwa chini ya Bodi ya wakurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Mloganzila wakiwemo wakurugenzi na viongozi waandamizi mara baada ya kuzindua miradi ya mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant) pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto ambao umelenga kukarabati wodi ya watoto wachanga mahututi (Neonatal ICU).
“Hospital hii imekuwa chini ya Bodi ya wakurugenzi wa hospitali ya Muhimbili kwa muda wa miaka minne sasa inatosha ikajitegemee yenyewe, ijisimamie kwa kujiendesha na kutoa huduma za matibabu kwa wananchi”. Amesema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa atahakikisha mchakato wa Hospitali hiyo kujitegemea unaharakishwa ili usiweze kukwamisha ifikapo Julai mosi.
Kwa upande wa uzinduzi wa miradi, Waziri Ummy amesema Mradi wa hewa tiba ya Oksijeni utasaidia kuzalisha mitungi 200 kwa siku na mradi wa pili umelenga kukarabati wodi ya watoto wachanga mahututi (Neonatal ICU) kwa msaada wa Serikali ya Korea.
Aidha, Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali imeamua kuanza kufanya uwekezaji kwa kusimika mitambo ya uzalishaji wa gesi tiba baada ya kuona changamoto za upatikanaji wake pamoja na gharama kuwa kubwa.
“Mwaka 2021 tumefanikiwa kufunga mitambo Saba katika Hospitali za Mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Amana, Geita, Mbeya, Manyara na Dodoma ambayo imeunganishwa moja kwa moja mpaka wodini aliko mgonjwa”. Amesema Waziri Ummy
Hata hivyo Waziri Ummy amesema Serikali ipo mbioni kukamilisha awamu ya pili ya ununuzi wa mitambo hiyo katika Mikoa kumi na mbili (12) kwa hospital za Rufaa ikiwemo Njombe, Songwe, Rukwa, Tabora, Kigoma, Mara, Simiyu, Morogoro Sokoine, Shinyanga, Katavi na Sekoe Toure.
Kwa upande wake Balozi wa Korea nchini Tanzania Mhe. Kim Sun Pyo amesema nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania hasa katika sekta ya Afya na kuahidi kusaidia katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
“Nchi ya Tanzania na Korea ilianza ushirikiano muda mrefu toka miaka ya 1992 kwa kusaidiana katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya na tutaendelea kufanya hivyo”. Amesema Balozi Kim.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...