Na. WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu ikiwemo kuwafikia wagonjwa na kutoa elimu ya ugonjwa huo kwa wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo Machi 21, 2022 wakati anakabidhi magari manne yatakayoratibu shughuli za Kifua Kikuu kwa Waganga Wakuu pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Shinyanga, Singida, Manyara na Morogoro katika viwanja vya ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema magari hayo yamepatikana chini ya udhamini wa Global Fund ambayo yamegharimu Shilingi Milioni 390 na kutaka yakatumike kwa kazi ya Ufuatiliaji na uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu katika maeneo yaliyokusudiwa.

"Kipaumbele cha magari haya ni kuongeza nguvu ya ufuatiliaji wa wagonjwa ya kifua kikuu lakini tunaweza tukayatumia katika mambo mengine ya shughuli za Afya kwa kuwa wote tunafanya kazi ya kuwahudumia watanzania". Amesema Waziri Ummy.

Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu 133,000 kila mwaka hali ambayo inahitaji nguvu zaidi katika mapambano.

"Mwaka jana tuliweza kuwafikia wagonjwa 87,000 sawa na asilimia 66, kwahiyo nafurahi kuona tunapiga hatua katika kupambana na ugonjwa huu wa kifua kikuu". Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa ushauri kwa watanzania endapo mtu ataona dalili za kifua kikuu kujitokeza mapema kupata matibabu kwa kuwa ni bure kwa wote.

Waziri Ummy amebainisha kuwa Kifua kikuu bado kimeendelea kuua watanzania lakini kinatibika ikiwa kitabainika mapema pamoja na kujikinga ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza maambukizi pamoja na vifo.

Tarehe 24 Machi 2022 ni maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu duniani na yanatarajiwa kufanyika kitaifa Mkoani Tanga.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...