Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

SERIKALI imetoa vipaumbele ili kuboresha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili kuliongezea uwezo na ufanisi katika Sekta ya Habari na Mawasiliano na kufikisha kwa Wananchi matangazo yake ya Radio na Runinga kwa ubora na usikivu mzuri nchi nzima.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Mhe. Nape Nnauye katika hafla ya kuzindua Jengo jipya la Studio za Televisheni (TBC2), amesema vipaumbele hivyo vilivyotolewa na Serikali kwa TBC ni kuwajengea uwezo wa Rasilimali watu, fedha, vifaa vya kisasa ili kuboresha zaidi utendaji kazi wao katika kuhabarisha, kuburudisha umma.

Mhe. Nape amewapongeza TBC kwa utekelezaji wake wa mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano, wa awamu ya tatu (2021-22 na 2025-26) katika kuwekeza zaidi kwenye Miundombinu ya Utangazaji (TBC), Upanuzi wa usikivu wa Radio, Ununuzi wa Mitambo na Vifaa vya Televisheni na Radio.

“Nawapongeza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 katika kuboresha Sekta ya Habari ili kurahisisha Wananchi kupata taarifa kwa urahisi”, amesema Mhe. Nape.

Aidha, Mhe. Nape amesema Serikali imekusudia kuimarisha zaidi miundombinu ya Utangazaji ya TBC kwa kuweka ‘Studio’ za kisasa za Televisheni na Radio katika Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ikiwa sambamba na kuimarisha usimamizi mzuri wa Shirika hilo katika kujiendesha kwake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayoub Rioba Chacha amesema ujenzi wa Studio hizo za TBC 2 umekamilika kwa Shilingi Bilioni 3.4 kwa kushirikiana na nchi ya Korea Kusini, baada ya makubaliano ya pande zote mbili za Tanzania na Korea Kusini.

“Tunawashukuru Korea Kusini kwa msaada mkubwa katika ujenzi wa ‘Studio’ hii ya TBC 2, Serikali yetu ya Tanzania imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 726 pekee katika ujenzi ambao umejumuisha Vyumba mbalimbali na ununuzi wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuzalisha maudhui bora kwa hadhira”, amesema Dkt. Rioba.

Naye, Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Sun Pyo Kim amesema ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu hiyo ya Shirika la Utangazaji Tanzania unaimarisha ushirikiano uliopo kati ya Korea Kusini na Tanzania, amesema uwepo wa Studio hizo za TBC 2 jamii itafikiwa na maudhui bora kutokana na ubora wa studio hizo sambamba na uwepo wa Wataalamu bora wa utangazaji na Waandaji wa vipindi mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayoub Rioba Chacha (wa katikati) akipewa hati ya makabidhiano na Mkurugenzi Mkuu wa GNTZ, Bi Soni Jung (wa kwanza kulia) kuashiria makabidhiano ya Jengo hilo la Studio za TBC 2.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza jambo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa jengo la Studio za TBC 2 Mikocheni jijini Dar es Salaam.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...