Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, leo Aprili 19, amewasili Kisiwani Pemba kwaajili ya Ziara maalum, ya Siku Nne.
Akiwa ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, wamepokelewa na viongozi mbali mbali wa kiserikali, vyama vya siasa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Mattar Zahor Masoud.
Akiwasalimia walimu na wanafunzi wa Skuli ya Utaani katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mheshimiwa Othman ameeleza azma ya Serikali, kutafuta mbadala wa Jengo lao la Asili lililoteketea vibaya kwa moto, mapema Mwezi wa Machi, Mwaka huu.
Aidha, Mheshimiwa Othman amependekeza kuwa, mbadala wa jengo hilo ni vyema ukazingatia umadhubuti wa asili sambamba na kujali miundombinu ya kuwezesha kuyakabili majanga kwa haraka, na ili pia kudumu kwa muda mrefu, kwa maslahi ya kizazi cha baadae.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Bw. Hamad Omar Bakar 'Small' amezishauri Mamlaka zinazohusika, kutumia busara ya kuzingatia vigezo maalum vya ufaulu wa mitihani inayokuja hivi karibuni, baada ya athari na changamoto kubwa zilizowapata wanafunzi hao, zikiwemo za kuteketea kwa vifaa vyao muhimu vya kujifunzia.
Katika ziara hiyo pia, Mheshimiwa Othman ametembelea Masoko ya Tibirinzi Chake Chake na Wete, kabla ya kuwa Mgeni Rasmi wa Hafla ya Ufungaji wa Mashindano ya Qur-an yaliyofanyika katika Kijiji cha Kiuyu M-buyuni, Mkoa wa Kaskazini, pia kisiwani Pemba.
Huo ni muendelezo wa ziara yake maalum, aliyoianza mwanzoni mwa Aprili 2022 kisiwani Unguja, ya kuwafariji na kuwapa pole wafiwa, wajane, wagonjwa na watu mbali mbali wasiojiweza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...