WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ihakikishe Watanzania wanaotoa ardhi yao waliyomilikishwa
kihalali kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo
uwekezaji wanalipwa fidia zao kwa wakati.
Amesema
hayo leo (Alhamisi, Mei 26, 2022) wakati akijibu swali la Mbunge wa
Tarime Vijijini, Mwita Waitara katika kipindi cha maswali ya papo kwa
papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina
mpango gani wa kuhakikisha wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na
wawekezaji wanalipwa fidia.
Amesema
ni muhimu kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia ulipwaji
wa fidia kwa wananchi waliotoa ardhi zao kwa shughuli za kimaendeleo.
”Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna madai yametolewa na hasa
kama uthamini umefanyika basi thamani ya ile ardhi iliyochukuliwa kwa
ajili ya kupisha shughuli nyingine ni lazima fidia ilipwe ili haki
itendeke”
Akijibu
Swali ya Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango
wa Serikali wa kupima maeneo ya Miji, Manispaa na Jiji, Waziri Mkuu
amesema kuwa mpango huo ni endelevu wenye lengo la kupima maeneo yote
nchini ili kubainisha huduma zote zinazotakiwa kutumika katika ardhi
hiyo.
Mheshimiwa
Majaliwa ameongeza kuwa mpango huo utakwenda hadi maeneo ya vijijini
ili kuwasiaidia kupata maeneo yaliyopimwa na kutambulika rasmi ili
waweze kupata hati. “Tunataka watumie hati hizi kama mtaji wa kukopea
kwenye taasisi zetu za fedha, lengo ni kila Mtanzania anufaike na ardhi
iliyopo, hivyo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iendelee
kukamilisha zoezi hili, hii itawasaidia hata wawekezaji kutambua maeneo
ya uwekezaji”
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha
wakulima wadogo wa chikichi waendelee kulima kwa wingi zao hilo lengo
likiwa ni kuhakikisha nchi inazalisha kwa wingi mafuta ya kula.
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kuwekeza kwenye kilimo hicho kwa kuwa nchi ina ardhi ya kutosha na yenye
rutuba. “Ardhi tunayo, na tumeshatoa maagizo kwa wakuu wa mikoa wote
kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji”
“Tunataka
tuzalishe na tukamue mafuta yetu sisi wenyewe, tunaamini gharama
itakuwa ndogo na zile fedha tunazotumia kuagiza mafuta nje hazitakwenda
tena bali tutaziingiza kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo,
uwekezaji huu ni mkubwa na endelevu”
Alikuwa
akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Assa Makanika ambaye
alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwakaribisha wawezaji wakubwa ili
kupunguza Nakisi ya kuagiza mafuta ya kula nchini.
Mheshimiwa
Majaliwa aliongeza kuwa, Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha
inaimarisha teknolojia inayotumika katika kukamua mafuta ya chikichi
“Sasa tunakwenda kuimairisha viwanda vya ukamuaji ili tuweze kukamua
asilimia 99 ya mafuta kwenye chikichi badala ya 70 ya sasa”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...