Wadau mbali mbali wa Afya na mashujaa wanaoishi na ugonjwa wa Lupasi, wakifurahia jambo kutoka kwa mgeni rasmi, Dkt. Pius Gerald ambaye ni Mkurugenzi wa Tiba Wizarani wakati wa maadhimisho akizungumza na wadau wa afya na mashujaa wanaoishi na ugonjwa wa Lupasi wakati wa maadhimisho ya siku ya Lupasi duniani, leo Mei 14, 2022 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tiba Wizarani, Dkt. Pius Gerlad, akizungumza na wadau wa afya na mashujaa wanaoishi na ugonjwa wa Lupasi (Hawapo pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya Lupasi duniani, leo Mei 14, 2022 jijini Dar es Salaam.


Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas),  Profesa Andrew Pembe akizungumza na wadau wa afya na mashujaa wanaoishi na ugonjwa wa Lupasi wakati wa maadhimisho ya siku ya Lupasi duniani, leo Mei 14, 2022 jijini Dar es Salaam
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia , Profesa Adolph Mkenda akizungumza na wadau wa afya na mashujaa wanaoishi na ugonjwa wa Lupasi wakati wa maadhimisho ya siku ya Lupasi duniani, leo Mei 14, 2022 jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja.

SERIKALI nchini Tanzania inatarajia kujenga kituo maalum pamoja na kuongeza wataalamu kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa Lupasi ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuutokomeza ugonjwa huo.

Hayo yameelezwa leo Mei 14, 2022, na Mwakilishi wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye ni Mkurugenzi wa Tiba wizarani, Dk. Pius Gerald wakati wa kuadhimisha siku ya ugonjwa wa Lupasi ambao huadhimishwa kila mwaka Mei 10.

Amesema kuwa watatengeneza mpango wa kutangaza ugonjwa huo ili watu waufahamu kwa lengo la kuondoa dhana potofu ikiwemo kurogwa na unyanyapaa pamoja na kuwapatia mafunzo madaktari namna ya kuutambua ugonjwa huo kwa haraka zaidi.

Amesema kuwa atapeleka mapendekezo Serikalini ya namna ya kuwa na kituo cha pamoja cha kutibu lupasi sambamba na kuongeza wataalamu kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa matibabu na vipimo vya ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa wametenga Sh. bilioni moja kwa ajili ya tafiti kwenye sayansi na tiba ili kutatua matatizo kwenye jamii.

"Tunaahidi wahadhiri watakaofanya tafiti na kuzichapisha kwenye majarida ya kimataifa watapatia Sh milioni 50 kila mmoja na tutawapatia ufadhili wa masomo ya nje kwa madaktari wetu. Lakini wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya sayansi hususani PCB na PCM tutawapatia ufadhili wa asilimia 100 kusoma bure haijalishi wazazi wao wanafedha au la lengo ni kuokoa maisha ya watu," amesema Profesa Mkenda.

Wakati huo huo Chama cha watu wenye Ugonjwa huo nchini kimeiomba serikali kuona namna ya kupunguza gharama za dawa na matibabu sambamba na kuweka kituo kimoja cha kutibu ugonjwa huo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Inakadiriwa kuwa kati ya watoto 52 waliopimwa ugonjwa wa lupasi, wanane ambao ni wakike sawa na asilimia 15 walikutwa na ugonjwa huo na kwamba kutokana na kutogundulika mapema na kuchelewa huduma za matibabu walifariki.

Mwakilishi wa wagonjwa hao, Siwazuri Mwinyi alisema huduma za matibabu pamoja na dawa hazijajumuishwa kwenye bima za afya hivyo kuwa mzigo kwa watanzania.

‘’Bei ya chini ya kidonge cha dawa za lupasi ni ghari mnoo kuna dozi inafika mpaka shilingi Milioni sita tunaiomba serikali itupunguzie gharama hizo’’ amesema Mwinyi.

Amesema kuwa zipo changamoto nyingi zinazowakabili wagonjwa wa lupasi ikiwemo kuchelewa kupata matibabu kutokana na kukosekana kwa wataalamu wenye ubobezi kwenye ugonjwa huo.

"Mpaka mtu anagundulika na ugonjwa wa lupasi anakuwa amezungukia katika hospitali nyingi na wengine huhusisha ugonjwa huu na imani za kishirikina sababu kubwa hakuna wataalamu. Kuna wagonjwa wa lupasi ambao walianza kutibiwa na kumeza vidonge vya Kifua Kikuu na wengine ngozi lakini kumbe ugonjwa wake ni lupasi," ameongeza Mwinyi.

Nay3, Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Profesa Andrew Pembe amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa katika jamii na watoa huduma za afya nchini.

Alisema kuwa bado kuna changamoto ya watalaamu wa afya wanaohudumia wagonjwa wa lupasi , kwani takwimu zinaonesha kuwa kati ya wagonjwa 100,000, 70 hadi 100 wanaugonjwa wa lupasi nchini.

Amesema kuwa ugonjwa huo unasababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa kinga ya mwili hivyo kushambulia kinga na kuathiri maeneo mbalimbal ya mwili ikiwemo figo, damu, mapafu, mgongo na ngozi.

‘’Changamoto kubwa ni vipimo vya ugonjwa huu kwani hupatikana kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Agakhan, TMJ, Hospitali ya Rufaa ya Bugando na KCMC. Wataalamu wengi wa afya huusisha ugonjwa huu na Ukimwi na TB hivyo, wataalamu wanaohudumia wagonjwa hawa ni wale madaktari bingwa na bobezi kwenye magonjwa ya figo, damu na mapafu,’’ amefanua Profesa Pembe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...