NA RAHIMA MOHAMED/ MAELEZO ZANZIBAR
Wizara ya afya inatarajia kujenga majengo mapya katika hospitali ya Rufaa Mnazimmoja pamoja na kuifanyia matengenezo jengo kongwe katika hospitali hiyo ili kuboresha zaidi huduma za Afya kwa Wananchi.
Hayo amesema Waziri wa Afya Mhe. Ahmed Mazrui wakati akizungumza na ugeni kutoka shirika la Badea huko ofisini kwake Mnazimmoja mjni Unguja walipofika kwa ajili ya kujadili maendeleo ya mradi wa ujenzi wa majengo mapya na kulifanyia ukarabati jengo kongwe.
Amesema mradi huo utasaidia kuweka mazingira mazuri zaidi ya hospitali hiyo kwani unaenda kuongeza idadi ya vyumba vya upasuaji,wodi za kulazia wagonjwa pamoja na sehemu za kutibia wagonjwa.
Aidha amesema mradi huo utasaidia kuongezeka upatikanaji tiba na kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya Afya kwa kutoa huduma bora kwa jamii.
" Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja itakuwa mpya yenye huduma zote muhimu za kuweza kuwahudumia wazanzibar "Alisema Waziri huyo.
Waziri Mazrui amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutaimarisha upatikanaji wa huduma nyingi za afya , kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kupunguza wimbi la wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Vilevile amesema kupitia mradi huo wataifanyia ukarabati mkubwa hospitali ya wazazi Mwembeladu kwa kuweka mazingira mazuri , kuweka vifaa vya kisasa pamoja na ujenzi mdogo katika hospitali ya wagonjwa wa akili kidongo chekundu utakaosaidia kuongeza matibabu hospitalini hapo.
Nae Sameh Azzuz mwakilishi kutoka shirika la Badea amesema shirika lake liko tayari kushirikiana na wizara hiyo ili kuhakikisha afya za wazanzibar zinaimarika.
Mwakilishi huyo ameahidi kukamilika mradi huo kwa wakati licha ya kusimama kwa muda mrefu kutokana na changamoto ya maradhi ya UVIKO 19.
Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Badea,na mfuko wa Quwait na Saudia Arabia ambapo jumla ya dola milioni 48 za kimarekani zitatumika kukamilisha ujenzi huo.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya Badea kuhusu mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja pamoja na ukarabati wa Jengo kongwe la Hospitali hiyo wakati walipofika Ofisini kwake kujadili maendeleo ya mradi huo utakaogharimu jumla ya dola milioni 48 kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakishirikiana na Badea,mfuko wa misaada wa Kuweit na Saudiarabia. PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Mwakilishi wa Badea Sameh Azzuz akizungumza na Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (hayumo Pichani) wakati alipofika Ofisini kwake kujadili maenedeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya rufaa Mnazimmoja pamoja na ukarabati wa Jengo kongwe la Hospitali hiyo utakaogharimu jumla ya dola milioni 48 kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakishirikiana na Badea,mfuko wa misaada wa Kuweit na Saudiarabia.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...