Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MIONGONI mwa mambo ambayo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) wamefanikiwa ni pamoja na kupeleka neema kwa wakulima wa Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kigoma.

WFP kupitia programu yake ya kusaidia wakulima kupitia Mradi wa Kigoma Pamoja (KJP) wamewezesha wakulima wengi kunufaika na kilimo hasa cha Maharage na Mahindi.Mradi wa Kigoma Pmaoja mbali ya WFP kuna mashirika mengine 16 Kwa pamoja ya kigoma.

Hata hivyo pamoja na Mradi wa Kigoma Pamoja kufanywa na mashirika hayo 16 mengi yakiwa ya Umoja wa Mataifa, WFP wao wameamua kuchukua eneo la kusaidia wakulima na hakika wamefanikiwa kuwasaidia na kiasi cha fedha zaidi ya Sh.bilioni tano imetumika.

WFP kupitia mradi huo umeshiriki katika masuala yanayohusisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima kulima kilimo cha kisasa lakini chenye kumnufaisha mkulima.Hivyo wakulima wamepata mafunzo kwa Awamu tofauti kuhusu kuanzia hatua ya uaandaji shamba, utunzaji wa shamba na mazao, uvunaji na uhifadhi wa mazao.Wakulima wamepata elimu ya kujua ni wakati gani sahihi wa kuvuna mazao na nini wafanye ili yabaki kuwa kwenye ubora ambao unakubalika kwenye viwango vya Kimataifa.


WFP hawakuishia hapo wametoa na fedha kwa ajili ya kukarabati maghala makubwa ya kuhifadhia mazao na hiyo ni baada ya kuona wakulima wanakosa mahali salama pa kuweka mazao yao baada ya kuvuna shambani.Maghala hayo yamejengwa katika maeneo mbalimbali katika Wilaya za Kasulu, Kibondo,Kakonko na Kasulu Mji .Wakulima wanao uhakika wa maeneo ya kuweka mazao yao.

Mbali ya kukarabati maghala WFP pia imenunua mashine Maalum ambazo wakulima wanatumia kwa ajili ya kupukuchulia mahindi.Ni mashine ambazo zimewasaidia wakulima kurahisisha upukuchuaji tofauti na ilivyokuwa awali.

WFP kupitia mradi huo wamejenga maeneo ambayo Wakulima wanatumia kuanika mazao yao baada ya kutoka shambani kwa Yale ambayo yanaonekana kutokauka vizuri, wamenunua maturubai ya kuanika mazao na kugawa kwa wakulima kupitia AMCOS zao .Hakika WFP wamebadilisha kabisa wakulima ambapo sasa wanalima kilimo chenye tija na kunufaika na kilimo hicho.


Kana kwamba hiyo haitoshi WFP wanaamini kwenye Umoja na mshikamano hivyo pamoja na mambo mengine walioamua kuwahamiza wakulima kujiunga kwenye AMCOS ili iwe rahisi kufikiwa na wakati huo huo kuwa na uwezo wa kupanga mipango yao inayohusu kilimo.Katika hilo wamefanikiwa sana wakulima wa Kigoma.Wanazo AMCOS imara sana na zenye kujua wakulima wanauhitaji nini na kwa wakati gani.

WFP pamoja na kufanya yote hayo kumuinua mkulima wa Kigoma na hasa katika maeneo yenye mradi, wameamua kuwa wanunuzi wa mazao ya wakulima hasa maharage na bei yao imefanya wakulima wawakimbilie.WFP wananunua kilo moja ya maharage Sh.1950 wakati wanunuzi wengi bei yao ni Sh 1400 au Sh 1500. Hata ingekuwa wewe ndio mkulima unadhani ungekimbilia wapi?

Siku za karibuni WFP iliamua kuwachukua waandishi wa habari na kuwapeleka Kigoma kwa lengo la kwenda kuona kile ambacho kimefanyika lakini pia kuonana na wanufaika wa mradi huo ambao ni wakulima.Hakika wakulima wanafurahia mradi huo ambao umekwenda kubadilisha maisha yao.

Wakati wakulima wakifurahia mradi huo, Serikali ya Mkoa wa Kigoma nayo imeeleza wazi namna ambavyo mradi wa Kigoma Pamoja ulivyopeleka maendeleo katika Mkoa huo lakini kwenye eneo la kilimo wanatoa shukrani kwa WFP.

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Rashid Mchata anaeleza namna ambavyo wakulima wa Mkoa huo na hasa Wilaya ambazo zimefikiwa na mradi huo wanavyonufaika.

"Kwa hiyo WFP kupitia program ya Kigoma Pamoja wamesaidia mambo mbalimbali hasa kwenye eneo la kilimo,wamesaidia katika ujenzi wa maghala Kuna uhitaji wa maghala kwa ajili ya wakulima wetu kwa hiyo tumebahatika, kwa mfano katika Wilaya ya Kasulu kuna maghala matatu wamesaidia kufanya ukarabati.

 "Katika Kijiji cha Nyakitoto, kijiji cha Kigadye na kijiji cha Kurugongo, kwa hiyo kuna vijiji vitatu katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu WFP wamesaidia kukarabati yale maghala na yanatumika na yanasaidia wakulima wetu.

"Pia wamesaidia katika  kuimarisha na kuanzisha vyama vya ushirika kama mnavyofahamu vyama vya ushirika kwenye mkoa wetu vilikuwa havijajienga vizuri , kwa hiyo WFP wamesadia sana kuanzisha na kuviweka vyama  vya ushirika hasa AMCOS, hivyo tumeona matunda ya kuwepo  vyama vya ushirika ambavyo vimesimama vizuri".

 Mchata ameongeza WFP wamesaidia kuunganisha vyama vya ushirika na masoko kwa hiyo wakulima Mkoa wa Kigoma wamekuwa na uhakika wa soko wanapotaka kuuza mazao yao .Kwa katika eneo la Nyakitonto WFP wameweza kununua mazao ya maharage mekundu.

"WFP wenyewe nao wamekuwa wanunuzi wa mazao ya wakulima , kama mnavyojua wamekuwa wakipika kwenye kambi za wakimbizi, kwa hiyo wamesaidia kununua mazao ambayo yapo kwenye AMCOS na yamefikia viwango yanafanyiwa vipimo na baada ya kuonekana yanafaa mikataba ikaingiwa.Kingine wamefanikiwa kuunganisha na wadau wengine kusaidia kwenye sekta ya kilimo.

"Katika jitihada za kumuinua mkulima, WFP imefanikisha kununuliwa kwa mashine za kupuchukulia mahindi ambapo vikundi mbalimbali wanavitumia.Pia  wamesaidia  maofisa ugani kufanya uuratibu katika shughuli za maofisa ugani na mikutano yao.Tunashukuru kwa mkoa wa kigoma uwepo wa wadau hususan WFP katika eneo la kilimo,"amesema

Mchata amesema WFP wamefanya kazi kubwa sana kwenye upande huo lakini na Serikali nayo imeanzisha program kama hiyo.Rais alizindua na akagawa vifaa kwa ajili ya maofisa ugani na sisi katika mkoa wao wa Kigoma kupitia WFP wana mifano ambavyo maofisa ugani wameweza kuwezeshwa kupititia hilo shirika, hivyo hata serikali inaweza kutumia mfumo huo.

Akielezea zaidi amesema mashirika 16 yaliyoko katika mradi wa Kigoma Pamoja yamekubaliana kutoa huduma kwenye kambi za wakimbizi  na maeneo ambayo yanazunguka kambi."Kwenye kilimo kuna mashirika ambayo unakuta yanahusika na kilimo, WFP wao wamejikita kwenye kilimo, kwenye afya unaweza kukuta mashirika mengine yanayohusika na afya.

Amefafanua mashirika hayo kila mmoja amechukua eneo lake,wako wanaoshughulika na elimu, maji, masuala ya kijinsia hasa kutokana na ukatili ulioko kwenye kambi za wakimbizi lakini ukatili unafanyika hata kwenye jamii."Kuna mashirika yanasaidia, kusomesha watoto ambao wamekosa elimu.Lakini kwa WFP wamejikita kwenye kusaidia eneo la kilimo.

Aidha mradi huo wa Kigoma Pamoja unakwenda kumalizika lakini Mkoa wa Kigoma ni matarajio yao WFP wataendelea na Awamu ya pili kutekeleza mradi huo hasa kutokana na tija yake kuonekana moja kwa moja na Kwa mujibu wa Mchata Mkoa nao umejipanga vema kuhakikisha wanaendelea na utekelezaji wa Yale yote yaliyoanzishwa na WFP kwani wanao watalaamu waliopata mafunzo mbalimbali kupitia programu hiyo ya Kigoma Pamoja.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...