Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaanza kugaharimia matibabu ya watoto 500 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kila mwaka.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi ambao wameshiriki mbio zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa Muhimbili(MOI) kwa lengo la kupata fedha za kuwatibu watoto 200 ambao wamezaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi.MOI wamekuwa na utaratibu wa kuandaa mbio hizo kila mwaka na kadri siku zinavyokwenda muamko watu kushiriki umekuwa mkubwa.

Waziri Ummy Mwalimu amesema hivi “sisi kama Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tutawaunga mkono MOI, leo mmetembea kwa ajili ya kuhakikisha watoto 200 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanawafanyiwa upasuaji.

“Kwa hiyo Serikali kuanzia mwakani tutagharamia watoto 500 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi , kwa hiyo 500 ukijulimisha watoto 200 wanahudumiwa na MOI kupitia fedha zinazopatikana kwenye mbio hizi tutakuwa kwa mwaka tunawatibu watoto zaidi ya 700 na hapo tunaamini idadi ya wananchi itaendelea kuongezeka katika kufanikisha kampeni hii.

“Kwa hiyo Rais Samia Suluhu Hassan amenielekeza Wizara ya Afya kuanzia mwakani tutagharamia watoto 500.Nitoe mwito kwa wazazi na walezi wasiwafiche watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi na badala yake wawapeleke kwenye vituo vya afya na hospitali ili wafanyiwe upasuaji  na wao waendelee na maisha yao ya kila siku,”amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha akielezea zaidi Waziri Ummy Mwalimu amesema watoto wanaozaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi ni tatizo kubwa nchini na takwimu zinaonesha katika nchi tano barani Afrika Tanzania ipo nafasi ya tatu kwa idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na matatizo hayo ikitanguliwa na nchi za Algeria na Ethiopia.

 

“Takwimu zinaonesha kwa Tanzania katika kila watoto 1000 watoto watatu wanazaliwa na tatizo hili la mgongo wazi na kichwa kikubwa kwa hiyo kwa mwaka tuna watoto takribani milioni mbili wanazaliwa nchini .Kwa hiyo ukichukua watatu katika kila watoto 1000 ni sawa sawa na watoto 6000 kila mwaka wanazaliwa na matatizo hayo.

“Na tatizo hili watalaamu wameeleza tunaweza kulizuia kwasababu vichwa vikubwa na mgongo wazi unatokana na ukosefu wa Folic acid ambayo inapatikana katika vyakula tunavyokula , baadhi ya vyakula hivyo ni Njegele, Maharagwe,Karoti, Machungwa ,mboga za majani pamoja na maboga.Kwa hiyo tunaweza kupata folic acid katika vyakula tunavyokula,”amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Ametoa mwito kwa wanawake wenye umri wa kuzaa kuanzia miaka 15 hadi miaka 49 hasa wale wanaopanga kupata watoto kuhakikisha miezi sita kabla ya ujauzito wawe wanakula vyakula vinavyoweza kuwapatia folic  acid.“Kwa hiyo nitoe mwito kwa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema kwnai kuna tatizo la wajawazito wengi kuchekelewa kwenda kliniki wakiwa na ujauzito,”amesema.

Aidha amesema kuna haja ya kuongeza folic acid ambazo zinatolewa bure na zinakuwa katika kidonge ambacho mhusika atakula kimoja kwa siku ,miezi sita kabla ya kupata ujauzito wako. “Kuna baadhi ya taasisi walikuwa wanataka tuzitoe kwa  wanafunzi lakini tukaona ni vema vidonge hivyo vikatolewa kwa wale wanapanga kubeba ujauzito.”

Pia amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za afya ya uzazi hususani kabla ya ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.“Lakini niwatake waganga wakuu wa mikoa na Wilaya kuhakikisha folic acid zinapatikana katika vituo vyote vya kutoa huduma kuanzia zahanati,vituo vya afya na kwenye hospitali.

“Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya mnapokwenda kuangalia huduma za afya , mnapokwenda kuangalia upatikanaji wa dawa, basi dawa ya kwanza ambayo nataka muiangalie baada ya chanjo ya watoto iwe folic acid kujua kama ipo.Pia nitoe rai kwa wakunga, madaktari na wauguzi mnapoona mtoto ambaye amezaliwa ana dalilia za kichwa kikubwa au mgongo wazi muwape rufaa mapema ili waweze kupata huduma mapema,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MOI Profesa Charles Mkonyi amesema wamefurahi kusikia Waziri wa Afya kuahidi kuwa mshiriki wa kudumu wa mbio hizo za kusaidia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ili wapatiwe matibabu.

“Pia tunashukuru kwa  jambo kubwa ambalo umelifanya siku za karibuni hapa MOI kwa kuiwezesha taasisi yetu kupata mashine mpya ya MRI na CT Scana , tunajua usumbufu unaotokea wakati mashine inapoharibika, sasa tunapokuwa na mashine za akiba hali yetu itakuwa nzuri, matatizo na changamoto zinazojitokeza wakati mashine inapoharibika tunaamini itakuwa historia,”amesema Profesa Mkonyi.

Aidha amesema pamoja na mafanikio yaliyopo katika kutoa huduma , bado wanazo changamoto kubwa ikiwemo ya kutoa matibabu kwa watu ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za tiba na hvyo MOI inalazimika kuzibeba kwa kutoa msamaha.

“Wagonjwa wanahitaji huduma hivyo inabidi tuwahudumie kwenye matibabu lakini hawana uwezo wa kulipia , taasisi ya MOI inatumia Sh.milioni 125  kwa mwezi kutoa msamaha kwa ajili ya kuwahudumia watu ambao hawana uwezo wa kulipia huduma, hii ina tafsiri Sh.bilioni 1.5 kwa mwaka fedha ambazo zinatumika na taasisi kwa ajili ya kuwahudumia watu ambao hawawezi kujiilipia.

“Kati ya fedha hizi watoto hawa wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambao ndio wametukutanisha hapa siku ya leo wanatumia kiasi cha Sh.milioni 46 kwa mwezi ambayo ni zaidi kidogo ya Sh.milioni 500 kwa mwaka kwani  wengi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu haya.

“Kutokana na hili tunaomba Serikali  yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara yako ione namna ya kusaidia taasisi kubeba mzigo huu wa matiba ya wenzetu ambao hawana uwezo wa kujilipia. Pia tunaomba watanzania wenye uwezo, kampuni na mashirika kushiriki katika kusaidia kuchangia matibabu kwa wenzetu ambao hawana uwezo wa kujilipia,”amesema Profesa Mkonyi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba na Mifupa(MOI) Dkt Respicious Boniface( wa tatu kulia) akizungumza mbele ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ( wa kwanza kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MOI Profesa Charles Mkonyi( wa  pili kushoto) wakati wa kuhitimisha mbio ambazo zimeandaliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanyia upasuaji Watoto wenye vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi wapatao 200.Washiriki wameshiriki kukimbia mbio za kilometa Tano, kilometa 10 pamoja na mbio kilometa 21.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza mbele ya washiriki wa mbio zilizoandaliwa na Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI) kwa lengo la kuchangisha fedha za kuwatibu Watoto 200 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kuanzia mwakani Serikali itakuwa ikigharamia matibabu ya Watoto 500 wenye matatizo hayo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MOI Profesa Charles Mkonyi akifafanua jambo wakati wa kuhitimisha mbio hizo zilifanyika leo Juni 26,2022 kuanzia saa 12 asubuhi.Ametumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kubeba jukumu la kugharamia matibabu ya wagonjwa ambao wanapatiwa huduma lakini hawana uwezo wa kulipia
Baadhi ya Watoto wenye vichwa vikubwa wakiwa mbele ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu baada ya kutoa shukrani zao kwa wote ambao wameshiriki mbio hizo kwa lengo la kukusanya fedha kusaidia matibabu yao.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (wa pili kulia) akiwa katika matukio ya picha mbalimbali alipokuwa akikabidhi vyeti kwa washiriki ambao wamekuwa sehemu ya kufanikisha mbio hizo
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (Katikati) akishiriki mazoezi ya viungo na washiriki wengine baada ya kumaliza kukimbia mbio za kilometa tano, kilometa 10 na kilometa 21.Waziri Ummy yeye amekimbia kilometa tano.
Matukio mbalimbali katika picha wakati washiriki walipokuwa kwenye mbio hizo zilizoandaliwa na Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI) kwa lengo la kukusanya fedha kusaidia matibabu ya Watoto wenye vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...