Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Makete yenye urefu wa kilomita 107 mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisalimia na Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda wakati Naibu Waziri huyo alipomtembelea Mkuu wa Wilaya hiyo Ofisi kwake, Wilayani Makete, Mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Ruth Shalluah wakati akimweleza maendeleo ya Barabara ya Njombe hadi Makete yenye Kilomita 107 iliyojengwa kwa kiwango cha Lami, Mkoani Njombe.
Serikali imesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Makete KM 107 kwa kiwango cha lami kumerahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mazao ya kilimo na mboga mboga kutoka shambani na kuelekea kwa walaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Njombe-Moronga yenye urefu wa kilometa 53 na kuwapongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kwa kusimamia ujenzi huo.
“Napenda kukupongea Meneja wa TANROADS kwa kazi nzuri unayoifanya ya kusimamia mradi huu na watalaam wako, nimeshuhudia mwenyewe kuwa viwango hapa vimezingatiwa niwaombe tu kwa kazi zilizo baki mzisimamie kwa karibu ili iwe ya mfano",amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na kukamilika kwa barabara hiyo amewataka TANROADS kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara kwani barabara hiyo ina kona nyingi ambazo bila elimu stahiki zinaweza kusababisha ajali kwa madereva wasio waangalifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda, amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa Wilaya imejipanga vilivyo kulinda miundombinu hiyo ambayo imejengwa kwa fedha nyingi.
Mkuu wa Wilaya hiyo ametoa rai kwa wananchi kutojihusisha na uhujumu wa miundombinu ya barabara hiyo kwani atakayebainika Wilaya haitosita kuchukua sheria juu yake.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe, Mhandisi Ruth Shalluah, amesema kwa ujumla ujenzi wa barabara hiyo umefikia zaidi ya asilimia 95 na kazi zilizobaki ni kukamilisha sehemu za mitaro na alama za barabarani.
Mhandisi Shalluah ameongeza kuwa tayari mkoa umejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara ili kupunguza ajali zinazoweza kujitokeza kwa sababu ya uzembe na kusema kuwa Wakala utaendelea na utaratibu wake wa ukaguzi wa mara kwa mara wa barabara hiyo ili kuhakikisha alama zinakuwepo muda wote.
Mradi wa Barabara ya Njombe hadi Makete yenye urefu wa KM 107 ambapo unatekelezwa kwa sehemu mbili ambazo ni sehemu ya kwanza kuanzia Njombe hadi Moronga KM 53 ujenzi wake umefikia asilimia 98 na sehemu ya pili ni Moronga hadi Makete ujenzi umefikia asilimia 96 na mradi wote umegharimu zaidi ya Bilioni 240.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...