Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Daniel Sillo (Mb) imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa miradi mitatu (3) ya miundombinu ya kitalii inayoendelea katika Pori la Akiba Mkungunero lililopo katika mikoa ya Dodoma na Manyara.
Tukio hilo lililofanyika jana tarehe 5 Julai, 2022, limehusisha ukaguzi wa miradi ya ujenzi ya barabara yenye kilometa 47.5, lango kuu la kuingilia wageni na eneo la kupumzikia watalii "picnic site" yote ikigharimu kiasi cha shilingi Milioni 672. Miradi hiyo imejengwa kwa kupitia fedha za Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti, Mhe. Daniel Sillo amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizi.
Aidha, Mhe. Sillo ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa usimamizi mzuri wa miradi hii na akasisitiza kuendelea kusimamia matumizi mazuri ya fedha za miradi ya maendeleo.
"Simamieni vizuri fedha za umma, ili zilete tija kwa kizazi cha sasa na baadae", Aliongeza.
Awali, Akizungumza wakati wa ukaribisho, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alisema uboreshaji wa miundombinu katika Pori la Akiba Mkungunero utatoa wigo mpana wa eneo hili kutembelewa na watalii kwa sababu ya miundombinu inayoendelea kuwekwa.
Kadhalika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka aliipongeza TAWA kwa nzuri na aliishukuru kamati kwa kutenga muda kwa ajili ya kupitia miradi hiyo.
Naye, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi ambazo zimetolewa kwa kipindi muafaka wakati Taifa likijiandaa kupokea wageni wengi baada ya uzinduzi wa filamu maalumu ya "Royal Tour". Aidha aliishukuru kamati kwa ushauri na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...