Serikali za Tanzania na Cuba zipo katika mchakato wa kupanua kiwanda cha Labiofam kilichopo Kibaha, Pwani cha kuzalisha viuadudu vya mazalia ya mbu ili kiwe na uwezo wa kuzalisha mbolea na dawa nyingine za kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.
Hayo
yamesemwa leo tarehe 12 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Maghembe wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya
Serikali za Tanzania na Cuba cha kujadiliana kuhusu upanuzi wa kiwanda hicho
kinachoendeshwa kwa ubia baina ya Serikali hizo mbili.
Dkt. Maghembe ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania unaojadiliana na ujumbe wa Cuba, alisema kuwa ana matumaini makubwa katika kikao hicho cha siku mbili, wajumbe watafikia makubaliano yatakayokuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.
“Kama unavyofahamu asilimia 70 hadi 80 ya Watanzania ni wakulima, hivyo, uwepo wa kiwanda hiki na uzalishaji wa mbolea na viuadudu ni fursa nzuri kwa wakulima wetu na nchi kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na wananchi kujipatia kipato kwa mazao watakayovuna”, Dkt. Maghembe alisema.
Kwa
upande wake kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa
Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez
alisema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni ishara ya wazi ya uhusiano mzuri uliopo
kati ya Cuba na Tanzania.
Aidha,
naye alielezea matumaini yake kuwa majadiliano hayo ya siku mbili yatakuwa na
faida kubwa kwa maendeleo ya sekta ya kilimo ya Tanzania na azma ya Serikali ya
kupamabana na ugonjwa wa malaria na hatimaye kuuangamiza kabisa.
Wataalamu wa Tanzania wanaoshiriki kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania |
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Maghembe (katikati), Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez (kulia) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Bw. Nicolus Shombe wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Cuba unaofanya majadiliano kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...