NA KHALFAN SAID, SABASABA
THAMANI ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) inakaribia trilioni 6 kulingana na mahesabu ambayo bado hayajakaguliwa yaliyoishia Tarehe 30/6/2022, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Masha Mshomba amesema.
Bw. Mshomba ameyasema hayo kwenye Banda la NSSF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere (maarufu Sabasaba) jijini Dar es Salaam Julai 3, 2022.
“Kwa sasa tuko trilioni 5.8 hiyo ndiyo thamani ya Mfuko na thamani hiyo imekuwa ikikua sana kufuatia mwitikio mzuri wa uchangiaji ambao waajiri wamekuwa wakionyesha kwa takriban miaka miwili iliyopita” alisema
Akifafanua zaidi Bw. Mshomba alisema, ” tunavyozungumza sasa hivi makusanyo ya mwezi yanazidi Bilioni 110.” Alibainisha.
Alisema mwaka ulioishia tarehe 30/6 NSSF ilikusanya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 (Trilioni 1 na bilioni 300).
“Hili ni ongezeko kubwa ukilinganisha na makusanyo ya mwaka uliopita ulioishia tarehe 30/6/ ambapo tulikusanya shilingi trilioni 1.1 (Trilioni 1 na bilioni 100), ongezeko la zaidi ya asilimia 18% hii inatokana na kwanza kuwajengea mazingira mazuri ya kazi watumishi yanayopelekea kuongezeka kwa ari ya kufanya kazi, matumizi ya TEHAMA yanayoziba mianya ya utendaji kazi usio wa kuridhisha, mwitikio wa waajiri na wafanyakazi,” Alifafanua.
Alisema Mfuko umekuwa ukiwapa waajiri elimu ya Hifadhi ya Jamii hali ambayo anaamini imesaidia kuongeza tija.
“Mtu akielewa umuhimu wa Hifadhi ya Jamii swala la mchango linakuwa sio la kumlazimisha kwasababu ndio njia pekee ambayo itampatia mtu kipato pale ambapo uwezo wa kufanya kazi unapokoma, Hifadhi ya Jamii unaweza kuona kama ni jambo dogo lakini umuhimu wake utauona unapofikisha umri wa miaka 60 ambao unastaafu au kwa bahati mbaya umepata ulemavu na usiweze kufanya kazi.” Alisema.
Lakini kama umewekeza kwenye Mfuko wetu mapato yako yako pale, watoto wako watapata, mwenza atapata na ndio maana sisi NSSF tunasema tunajali maisha yako ya sasa na ya baadaye, alisema.
Kwa upande wa ulipaji Mafao, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema mwaka jana NSSF ililipa Mafao shilingi bilioni 594 na wanajiandaa kulipa shilingi bilioni 658 mwaka unaofuata ambapo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 10%.
“Mwitikio ni mkubwa lakini tunaweza kulipa sana kwa sababu wanaoomba kulipwa Mafao ni wengi lakini pia matumizi ya TEHAMA yanasaidia sana.” Alisema na kuongeza.. “Ndio maana tunasema siku za usoni sisi dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba tunatumia TEHAMA kwa matumizi yetu yote.
ULIPAJI KODI YA SERIKALI
Kwa upande wa serikali NSSF imekuwa ikisaidia sana kupitia ulipaji kodi za serikali, katika miaka mitano iliyopita NSSF imelipa kodi zaidi ya shilingi bilioni 400,
“Kiwango hiki sio ndogo kodi hiyo inasiadia katika kuchangia maendeleo ya taifa ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali, shule.
Lakini pia NSSF imekuwa ikisaidia jamii kupitia (Corporate Social Responsibility) ambapo alisema kuna sera mahsusi inayowaelekeza kujikita katika mambao ya msingi kama vile Afya, Elimu, Barabara na wamekuwa wakifanya kazi kubwa kupitia mpango huo.
Kuhusu ushiriki wa Mfuko kwenye Maonesho hayo, alisema ni fursa nzuri ya kukutana na wadau ili kutoa elimu ya masuala mbalimbali yahusuyo Hifadhi ya Jamii lakini pia kuwahudumia wanachama na wananchi kwa ujumla.
Katika Maonesho haya tumekuwa tukitoa elimu kuhusu Kikokotoo kipya.
“Tunatoa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ambayo yametokea katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kama mnavyofahamu kumekuwa na mabadiliko ya kikokotoo namna ambavyo tunawalipa wastaafu wetu kuanzia tarehe 1/7/2022, tumebadilisha kidogo fomula ya ulipaji.
Jambo hili lilikuwa la muda mrefu tangu serikali ya awamu iliyopita mwaka 2018 yalitoka maagizo ya kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikisha wadau wa vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali.
Uamuzi huo wa serikali ni kufuatia malalamiko yaliyotokea baada ya ile fomula iliyowekwa kufuatia mabadiliko ya sheria ya mwaka 2018
Tunashukuru kwa jitihada kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Jambo hilo limewezekana na kuanzia tarehe hiyo tuna fomula mpya ya ulipaji Mafao.
Katika hili kwakweli tunampongeza sana Mhe. Rais, jambo hili litabaki katika historia kama moja ya Legacy yake, na nimpongeze pia Mhe. Spika Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika na Wabunge kwa ujumla kwa kufanya kazi kubwa ya kulijadili swala hili kwa kina na ninahakika Waheshimiwa Wabunge watakaporudi kwa wananchi huko majimboni watakuwa wawakilishi wazuri sana kuwaelezea wananchi kuwa jambo hili lina umuhimu mkubwa kwa taifa.
“Kufuatia mabadiliko hayo NSSF sasa italipa malipo ya mkupuo asilimia 33% badala ya asilimia 25% ya fomula ya zamani kwa hiyo ni jambo zuri na wananchama wamelipokea vizuri na maisha ya wananchama yataendelea kuboreka.” Alisema.
Matumizi ya Mifumo (TEHAMA)
Pia tunasisitiza sana matumizi ya Mifumo ndani ya NSSF, takriban miaka miwili sasa tumekuwa tukitoa kipaumbele shughuli zetu zote za msingi tunazifanya kwa kutumia mifumo, jambo hilo ni muhimu kwa sababu kwanza linaboresha huduma lakini pia linatupunguzia gharama za uendeshaji na wateja wamekuwa wakifurahia kwa sababu linawapa urahisi wa kufanya mambo yao na wengi hawahitaji kuja katika ofisi za NSSF, huko waliko wnaaweza kutumia simu zao au komputa wakaingia kwenye website ya NSSF na kupata huduma zetu bila ya kuhitajika kufika ofisini kwetu.
Nijambo tulilolipa kipaumbele na tunatumia maonesho haya kuzidi kuwaelkimisha wanachama wetu na wananchi kwa ujumla kuhusu matumizi ya TEHAMA na tunawaahidi kwamba hata kwa zile shughuli chache ambazo hazijawekwa katika mfumo, ndani ya mwaka mmoja huu unaokuja tunatarajia kwamba tutakuwa tumeziweka katika mfumo na tunatumaini tukifikia hatua hiyo huduma zetu zitaboreka sana na ndivyo dunia inavyokwenda na sisi NSSF tunataka kwenda kidijitali na tunataka iwe ya kidijitali kwelikweli.
TUNATOA HUDUMA ZA KAWAIDA
Tuko hapo kwa ajili ya kutoa huduma pia mtu akija kuulizia michango yake, akitaka kujua hatua ya mafao yake yamefikia hatua gani
weze kulipwa, pia akitaka kujisajili kama amekidhi vigezo tuko hapa kumsajili na vile vile tunatumia nafasi hii kutatua kero wengine wakija si kwamba wanataka kuhudumiwa tu lakini wanakuwa na kero zao kwa namna moja au nyingine tunatumia nafasi hii kutatua kero kwa kadiri ambavyo mazingira yaliyopo hapa, kama yatashindikana tutamuelekeza kushughulikia kero hiyo kwenye ofisi zetu.
UWEKEZAJI
Kutangaza shughuli zetu za kiuwekezaji, kama mnavyojua NSSF ni moja ya taasisi kubwa hapa nchini zinazowekeza kwa kiasi kikubwa sana, tunatumia nafasi hii kutangaza uwekezaji wetu nyumba zetu za kupangisha na kununua mfano tuna nyumba huko Wilayani Kigamboni hususan Mtoni Kijichi, Tuangoma, Dungu, maeneo ya Muongozo.
Tuna nyumba nzuri sana na mwitikio wa kununua nyumba hizo umekua ni mzuri sana, pia tunajenga jengo la Mzizima hapa Dar es Salaam na nia hasa ni kulipangisha kwa watu watakaoendesha mradi wa hoteli pia Mwanza na lengo ni hilo hilo kulipangisha kwa mtu atakayeendesha shughuli za hoteli, tunatumia Maonesho haya kutangaza hizo nafasi ndani ya nchi lakini pia nje ya nchi ili tuweze kupata wadau hao ili kuhakikisha tunapata wapangaji au kununua nyumba hizo.
Mkurugenzi Mkuu NSSF, Bw. Masha Mshomba (kushoto), Meneja wa Mpango wa Sekta Isiyo Rasmi wa Mfuko huo, Bi. Rehema Chuma (watatu kushoto) na Meneja wa Mfuko huo Mkoa wa Temeke Bw. Feruzi Mtika, wakimsikilzia Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma NSSF, Bi. Lulu Mengele wakati kiongozi huyo alipotembelea banda la NSSF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Julai 3, 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, akimsikiliza Mfanyakazi wa Mfuko huo anayesimamia masyala ya uwekezaji.
Bw. Mshomba akimsikilzia Afisa Matekelezo Mkuu, NSSF, Bi. Asha Salum
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...