*
Serikali yatoa maagizo utekelezaji yaliyotolewa na Makamu wa Rais ili
kuendana na kasi ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani
LUGHA
ya Kiswahili imeendelea kutandawaa ulimwenguni kote baada ya toleo
jipya la kamusi ya lugha ya kiingereza ya Oxford kuingiza maneno ya
Kiswahili takribani mia mbili tofauti na mwaka juzi ambapo kamusi hiyo
iliingizwa maneno ya Kiswahili matano pekee.
Hayo
yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa
(BAKITA,) Bi. Consolatha Mushi wakati akitoa mkakati wa utekelezaji wa
maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzanaia Dkt. Philip Mpango katika siku ya maadhimisho ya siku ya
Kiswahili ulimwenguni iliyofanyika Julai saba mwaka huu na kuelekeza
kuanza rasmi kwa utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuendana na
maendeleo yake ya kasi ulimwenguni.
''Tunafahamu
kamusi ya Oxford inatumika sana duniani, ni kamusi ya kiingereza ila
katika toleo hili imehusisha maneno ya Kiswahili mengi zaidi, hii ni
tabia ya lugha ya kuchota maneno katika lugha nyingine, na inatupa
fahari kubwa na inadhihirisha kuwa Kiswahili kimefika mbali.'' Amesema.
Amesema
baadhi ya maneno yaliyoingizwa katika kamusi hiyo ni pamoja na neno
'daladala' likimaanisha magari yanayotumika kusafirisha abiria na 'jembe'
kifaa kinachotumika kulimia.
''Maneno
yaliyoingizwa katika kamusi hii na kuwa rasmi ni maneno yaliyozoeleka
kimatumizi, neno 'chapo' likimaanisha chapati linalotumika sana
nchini Kenya limeingizwa katika kamusi hiyo, pia neno 'Mama Ntilie '
limeingizwa katika kamusi ya Oxford kwa maana ya Mama anayepika chakula
na kuwauzia watu kwa gharama nafuu ili kila mtu aweze kumudu na kupata
chakula, aidha neno 'Singeli' limechukuliwa kama muziki ambao asili yake
ni Tanzania, neno 'Kolabo' na 'sambaza' pia yameingizwa katika Oxford...Hii ni
dhahiri kuwa Kiswahili kwa sasa kinaenda kwa kasi kubwa.'' Amesema.
Aidha
amesema kuwa, Kiswahili kinazungumzwa na watu wapatao milioni 500
duniani msamiati wake unakua na kukuza lugha nyingine na kuingizwa kwa
maneno hayo katika kamusi ya Oxford kutasaidia katika kusambaza msamiati
wa Kiswahili pamoja na utamaduni wa Mswahili.
''Neno
jingine lililoingizwa katika kamusi ya Oxford ni 'chips yai', wengi
watataka kufahamu chakula hiki cha chips yai kipoje na kinatengenezwaje
tayari tumepeleka utamaduni wa vyakula katika lugha ya kiingereza..Hii
ni tija kubwa na fahari kubwa mabaraza yapo kwa ajili ya kutengeneza
msamiati ili kusonga mbele zaidi.'' Ameeleza.
Amesema
kuwa mabaraza yaliyoundwa kisheria yataendelea kufanya usanifishaji na
utafiti mkubwa wa kuchukua maneno mengine ya lugha za kiafrika na
kuyaingiza katika lugha ya Kiswahili.
Akitoa tamko juu hatua ya kuanza utekelezaji wa maagizo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili
yaliyotolewa na Makamu wa Rais Dk. Philiph Mpango, kwa niaba ya Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa Bi. Consolatha
amesema kuwa
maagizo hayo yanayotakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia sasa
ni pamoja na nyaraka za Serikali kati ya ofisi moja na nyingine, idara
na idara, taasisi za Umma na binafsi na mashirika kuandikwa kwa
lugha ya Kiswahili na ikiwa nyaraka hizo zinaandikwa kwa mgeni nyaraka
mbili za kiingereza na Kiswahili zitumike.
''Makamu wa Rais pia ameelekeza katika majina ya barabara, mitaa na
majina ya vifaa mbalimbali yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili..Katika
zoezi linaloendelea nchini la kuweka majina ya mitaa tumeona lugha
inayotumika pengine inakosewa hivyo agizo la Makamu wa Rais la kuandika
majina ya mitaa kwa lugha ya Kiswahili lizingatiwe na lugha
itakayoandikwa iwe fasaha na sanifu..Baraza lipo tayari kutoa msaada wa
kuhakiki majina hayo.'' Amesema.
Aidha amesema maeneo mengine ambayo utekelezaji wake
unapaswa
kuanza mara moja ni pamoja na mabango ya matangazo yote yaliyopo
barabarani kuwa katika lugha ya Kiswahili, maelezo ya bidhaa zote
zinazozalishwa viwandani,fomu za usahili pamoja maelezo ya matumizi ya
dawa yawe kwa lugha ya Kiswahili ili kuweza kumlinda mlaji dhidi ya
athari hasi zinazoweza kutokea kwa kushindwa kuelewa maelezo
yaliyotolewa.
''Miradi
yote inayohusu wananchi lazima iandikwe kwa Kiswahili ili kuwasaidia
wananchi kuelewa miradi hiyo, sheria na kanuni zinaendelea kutafsiriwa
kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Baraza ili kukipeleka
Kiswahili mbele zaidi..BAKITA na BAKIZA tunaendelea kusimamia
utekelezaji wa maelekezo ya maagizo hayo.'' Amesema.
Aidha
amevitaka vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuzingatia
agizo la Makamu wa Rais la kuzingatia matumizi sahihi na fasaha na
sanifu ya Kiswahili na wakishindwa watumie mabaraza ya kuelekezwa
matumizi fasaha ya lugha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...