Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MKURUGENZI wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba(TMDA) Adam Fimbo amesema wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza dawa bandia, pamoja na dawa duni.
Akizungumza leo Julai 5,2022 na Michuzi TV na Michuzi Blog katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Dar es Salaam Fimbo amesema kuna mafanikio makubwa katika kudhibiti dawa bandia kuingia nchini.
Amefafanua kupitia operesheni na mifumo kuanzia usajili , ukaguzi na udhibiti maeneo ya mipakani wanaona mafanikio makubwa na kwamba katika kipindi cha miaka mitatu nyuma walikuwa katika asilimia tatu lakini hivi sasa ni asilimia moja.
“Na sasa hivi kiasilimia tukiangalia kati ya miaka mitatu iliyopita dawa bandia ilikuwa iko kwenye asilimia tatu , wakati takwimu za Shirika la Afya duniani kwa Afrika nzima ilikuwa asilimia 30.
“Sisi kwa Tanzania ilikuwa asilimia tatu katika kipindi cha miaka mitatu lakini kutokana na juhudi tunazofanya tuko asilimia moja ya uwepo wa dawa bandia na hicho ndio kiashiria kikubwa cha sisi kuona mifumo inafanya kazi.
“Kwetu sisi ni kipimo kuona kama mifumo je inafanya kazi? Kwasababu kama haifanyi kazi uwepo wa dawa bandia kwa mfano au dawa duni kwenye soko ungekuwa mkubwa.
“Lakini ukiona unafanya vipimo vyao halafu dawa bandia na dwa duni zimepungua maana yake mifumo inafanya kazi.Dawa ambazo ziko katika maduka ya dawa ni zile ambazo TMDA imezithibisha , imepitia ubora wake, usalama wake, imepitia utafiti wake,amesema.
Amefafanua kwa hivyo dawa ambazo zinatumiwa na wananchi zinafaa kwa matumizi ya binadamu pamoja na mifugo kwa zile dawa za mifugo, kwa hiyo wakiangalia matukio yamekuwa machache.
“Unajua TMDA ni taasisi ya kwanza barani Afrika kwa udhibiti , tunafanyiwa uhakiki mara kwa mara na Shirika la Afya Duniani na wametuona tuko vizuri kwenye mifumo yetu.
“Tunaishukuru Serikali imetupa watumishi wa kutosha, tunao wachunguzi wengi kwenye maabara zetu wanafanya uchunguzi wa ubora wa dawa na vifaa tiba. Uwekezaji umekuwa mkubwa.
“Na sasa tumefungua ofisini nyingine Dodoma, rasilimali ziko za kutosha ili kuwa na mfumo thabiti ambao utawezesha kudhibiti dawa bandia kwa ajili ya usalama wa binadamu.
“Kwa hiyo niseme kwa kipindi hiki ambacho tumekuwa tukisimamia hizi kazi tunakwenda vizuri na ushiriki wa wananchi ni mkubwa sana na wamekuwa wakisaidia kutuelezea na kisha tunachukua hatua,”amesema Fimbo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...