Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali kupitia wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea na ujenzi wa bwawa la maji katika kijiji cha Msomera kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.99 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15 na Ujenzi huo utakapokamilika, utasaidia kuboresha huduma ya maji kwa wananchi pamoja na mifugo.

RUWASA inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji hicho, ambapo mpango wa utekelezaji uligawanywa katika awamu mbili (awamu ya muda mfupi na awamu ya muda mrefu),Ambapo awamu ya muda mfupi imekamilika na vituo vya kuchotea maji 12 vimeshaanza kutoa huduma ya maji, awamu ya pili imefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2022.

Akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 mbele ya waandishi wa habari Julai 18,2022 jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo amesema kuwa Sambamba na utekelezaji wa mpango wa bajeti 2021/2022, kuliibuka pia uhitaji wa mradi wa maji kwa wananchi wa Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni ambacho wananchi kutoka Ngorongoro walihamia kwa hiari hivyo ikawalazimu kuwekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha wanapata maji.

Ameseama kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 17,000 pamoja na mifugo yao na kupelekea idadi ya vituo vya maji kuongezeka kutoka 12 hadi kufikia vituo vya kuchotea maji 30 kwa matumizi ya binadamu na vituo 3 vya kunyweshea maji mifugo.

"Niwahakikishie tu wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera kuwa hawatapata changamoto yeyote ya maji hivyo ambao bado hawajahamia wafanye hivyo kwa uhakika RUWASA imedhamiria kuondoa kabisa tatizo la maji katika vijiji vyote na kusaidia kukamilisha adhma ya Mhe.Raisi ya kumtua mama ndoo Kichwani"amesema Mhandisi Kivegalo

Mhandisi Kivegalo amesema kuwa kwa sasa, kati ya vijiji vyote nchini 12,319 ni vijiji 8,769 vinavyofikiwa na huduma ya uhakika ya maji safi na salama.

"Kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika mwezi Aprili, 2022 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa umefikia kiwango cha asilimia 74.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na wastani wa 64.8 mwaka 2019"Amesema Mhandisi Kivegalo

Na kuongeza "Kasi hii, ni nzuri na tukienda kwa kasi hii, tunatarajia kuvuka lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi"

Ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia RUWASA ilipanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji 1,527, ambapo kati ya hiyo, miradi 1,176 ilikuwa ni ujenzi wa skimu za usambazaji maji, miradi 351 ilikuwa ni ya utafutaji wa vyanzo vya maji chini ya ardhi na miradi 19 ilikuwa ni ya usanifu na jenzi wa mabwawa, ambayo baadaye hutumika kama vyanzo vya maji.

Mhandisi Kivegalo ameleza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya miradi 303 ilikuwa imekamilika na miradi 873 ilikuwa inaendelea na utekelezaji,Miradi 225 kati ya miradi iliyokuwa inaendela na utekelezaji inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2022 na miradi 648 itaendelea na utekelezaji. Kukamilika kwa miradi 303, kumewezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 1,467,107 kupitia vituo vya kuchotea maji 4,147 vilivyojengwa katika maeneo ya vijiji mbalimbali.

Katika mwaka huu wa fedha 2022/23, RUWASA imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,029, ambapo kati ya miradi hiyo 381 ni mipya na miradi 648 ile ambayo utekelezaji wake unaendelea kutoka mwaka wa fedha uliopita. Kiasi cha Sh. 387,736,591,242. kimeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kuongezeka kwa wastani wa asilimia 6.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa katika sekta ya maji Mhe.Rais ameahidi na anaendelea kutekeleza kauli mbiu yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa sababu bila maji hakuna jambo lolote la kijamii au kimaendeleo linaloweza kuendelea ndio maana RUWASA wanapambana usiku na mchana kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji kwa uhakika.

"Kwanza niwapongeze RUWASA kwa sababu tangu kuanzishwa kwa mamlaka hii imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kuhakikisha vijiji ambavyo hawakuwa na huduma za maji vinapata maji na kwa kweli kazi yenu inaonekana na matokeo yake imemfanya Mhe.Rais kuongeza bajeti ya wizara ya maji ili kuendelea kuongeza tija ya upatikanaji wa maji kwa wananchi "Amesema Msigwa
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo Akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 mbele ya waandishi wa habari Julai 18,2022 jijini Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari Julai 18,2022 jijini Dodoma baada ya wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023
Sehemu ya waandishi wa habari waliojitokeza katika mkutano huo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo Julai 18,2022 jijini Dodoma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...