Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mfano wa jengo, kwenye banda la Chuo Kikuu cha Ardhi, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam .

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza Watendaji wa Wizara ya Elimu na Tume ya Elimu ya Juu Tanzania (TCU), baada ya kufungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022. Kutoka kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa, Mwenyekiti wa Bodi Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Penina Muhando na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa James Mdoe.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia ndege isiyokua na rubani inayotumika kupiga picha za anga kwa ajili ya kuandaa ramani za msingi zinazowezesha kupanga miji, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam .


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kompyuta mpakato inayotumia mwanafunzi ya Chuo Kikuu Huria, mwenye uono hafifu Bernadeta Msigwa kwa kuandikia vitabu, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam .


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea ngao ya shukrani kwa kufungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Na karama Kenyunko, Michuzi TV 
WAZIRI MKuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim  Majaliwa ameziagiza taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha wanatoa elimu yenye ubora unaostahili itakayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii  na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Pia amewaasa kuendelea kufanya mapitio ya mitaala yao kwa kuzingatia miongozo iliyopo Ili  kusaidia wahitimu wa vyuo vikuu  kuendana na mahitaji ya soko la ajira .

Majaliwa amesema hayo leo Julai 19, 2022 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 17 ya vyuo vikuu jijini Dar es Salaam.

Amesema taasisi hizo hazina budi kwenda na wakati kwa kuhakikisha zinabuni programu mpya zinazoenda na wakati ili kutoa wigo mpana Kwa wanafunzi wenye mawazo ya tafiti na ubunifu wenye manufaa kwao.

Maonesho hayo ya 17 ya vyuo  vikuu yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Elimu ya Juu inayokidhi Mahitaji ya Soko la Ajira Kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi". Kaulimbiu hiyo inatoa changamoto kwa Taasisi za Elimu ya Juu  nchini kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa na taasisi hizo inawapa wahitimu maarifa na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.

"Tukumbuke kuwa tunapoongelea soko la ajira, tunamaanisha ama ajira ya kuajiriwa Serikalini, Sekta binafsi au kujiajiri. Hivyo ni lazima wahitimu wetu wawe na maarifa na ujuzi wa kuweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe ili kuweza kuboresha hali zao za maisha na kuchangia katika ujenzi wa uchumi na maendeleo ya taifa letu" amesema Majaliwa.

Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali imeongeza wigo wa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi zaidi wanamudu gharama za masomo ya Elimu ya Juu. 

Aidha Majaliwa ametaja tathimini ya Serikali iliyofanywa na Tume ya Mipango mwaka 2014 kuhusiana na hali ya soko la ajira na ujuzi unaotolewa kwenye taasisi za  elimu utakaoifanya Tanzania kuwa na uchumi imara na shindani ifikapo mwaka 2025 .

Waziri Mkuu amesema tathimini hiyo imebaini kuwa viwango vya  ujuzi wa watafuta ajira vipo chini ya kiwango kinachohitajika kwa waajiri.

Waziri Mkuu amesema kuwa tathimini hiyo ilibaini  upungufu kwa wahitimu kwenye soko la ajira ni pamoja na kukosa ubunifu 

"Mapungufu yaliyobainishwa ni pamoja na uwezo mdogo kwenye mawasiliano, wahitimu kushindwa kujiamini, kukosa ubunifu, kutojituma katika kutatua changamoto,  udhaifu katika uongozi na uwezo mdogo wa kutumia nadharia katika vitendo, matumizi mabaya ya muda, kutokumjali mteja na kukosa mtazamo chanya kufanya kazi kwa kushirikiana na wengine." Amesema.

Amesema kuwa Tathimini hiyo imetoa muelekeo kwa Taasisi za elimu ya juu kutathimini mifumo yao ya utoaji elimu ili kwenda sambamba na mabadiliko. 

Amesema kuwa Serikali imeamua kupitia upya sera ya taifa ya elimu ili kufanya maboresho ya mfumo wa elimu kuanzia ngazi ya chini mpaka elimu ya juu.

"Sote tunafahamu elimu ya juu ina mchango kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa lolote Duniani kauli mbiu hii imeletwa wakati sisi kama taifa tumeanza na tunaendelea na mchakato wa mapitio ya sera yetu ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014." Ameeleza.

Amesema kuwa mapitio hayo yatahusisha ngazi zote za kielimu husasani ile ya Chekechea, elimu ya msingi , Sekondari, elimu ya kati juu mpaka vyuo vikuu.

Amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha elimu inayotolewa inaubora na inakidhi mahitaji ya soko la ajira itakayokuwa chachu ya maendeleo kwa jamii na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya vyuo vikuu Profesa Penina Mhando amesema, maonesho hayo ambayo yamekuwa yakiandaliwa na TCU kila mwaka tangu mwaka 2016 yamekuwa yakitoa fursa kwa Taasisi za elimu ya juu kutangaza huduma na kazi wanazozifanya  kwa nia ya kuleta ustawi wa elimu ya juu katika Teknolojia, uchumi na Maendeleo ya jamii.

Amesema maonesho hayo pia yanalenga kujenga na kuimarisha mahusiano  baina ya Taasisi za elimu ya juu. 

"Tutaendelea kuhakikisha kuwa maonesho haya yanakuwa chachu ya kuongeza fursa ya masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu wa ndani na nje ya nchi na kuchagiza ushindani baina ya Taasisi zinazoshiriki kwa lengo la kuinua viwango vya ubora wa elimu ya juu", Amesema Profesa Malama.

Ameongeza kuwa TCU itaendelea kusimamia na kuimarisha mifumo ya udhibiti bora wa elimu ya juu ili kuzifanya Taasisi za elimu ya juu kuwa chachu ya Maendeleo ya Taifa kwa kuzalisha wahitimu mahiri wabunifu na wenye uwezo wa kustahimili ushindani wa soko la ajira na kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Awali Katibu Mtendaji wa TCU Charles Kihampa  alieleza kuwa,  kwa mwaka huu jumla ya Taasisi 75 zimeshiriki ikilinganishwa na Taasisi 74 zilizoshiriki Maonesho mwaka jana 16 

"Taasisi zinazoshiriki Maonesho ya mwaka huu zinajumuisha taasisi zinazotoa mafunzo kwa ngazi ya elimu ya juu zipo Taasisi 55 mabaraza ya udhibiti ubora mawili, wakala na Taasisi zingine za Serikali ziko tatu bodi za usajili wa wataalamu, Taasisi za Sayansi teknolojiana utafiti iko moja na Taasisi za huduma za kifedha na wakala wa vyuo vikuu vya nje nchini tisa." Amefafanua Kihampa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...