WAZIRI wa Nishati January Makamba amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO,) kwa kuwa shirika la kihuduma zaidi kwa mawasiliano, elimu na huduma kwa Umma kwa kuwasiliana na kuwafikia wananchi sambamba na kupokeo kero, changamoto na maoni ya wananchi na kuyapatia uvumbuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la TANESCO katika maonesho ya 46 ya kimataifa ya biashara maarufu kama Sabasaba Makamba amesema kuwa, Wizara na taasisi wameshiriki maonesho hayo ili kutoa elimu kwa Umma wa Tanzania kuhusiana na majukumu yanazofanywa na Wizara na Taasisi wanazozisimamia pamoja na huduma zinazotolewa.
''Tukiwa kama Wizara, Serikali na taasisi ni jukumu letu kuhakikisha mawasiliano kwa Umma na Umma ni muhimu ili wananchi waweze kuelewa ni nini tunafanya na hatua zinazochukuliwa na wizara katika kuboresha huduma zinazotolewa na wizara pamoja na taasisi zake.'' Amesema.
Makamba amesema amefarijika baada ya taasisi hizo na viongozi wake kushiriki kwa ukaribu zaidi na kuwahudumia wananchi katika maonesho hayo kwa ukamilifu akiwemo Mkuregenzi mkuu wa TANESCO Maharage Chande.
''Tunaona namna suala hili lilivyo muhimu kwa Wizara na taasisi zote, mawasiliano, elimu na huduma kwa Umma ni muhimu kwetu tunamwona MD Chande yupo hapa akishiriki kutoa huduma kwa wananchi hii ni namna ambayo tumejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi anapata na kufikiwa na huduma kwa kiwango bora zaidi.'' Ameeleza.
Waziri Makamba ameeleza kuwa TANESCO ni shirika linalobadilika na limejipanga katika kuboresha huduma na kurahisisha upatikanaji wa umeme na kusambaza umeme kwa gharama nafuu nchi nzima.
''Ninafarijika na mwenendo wa shirika, limekuwa zaidi ya shirika la kiufundi na uhandisi na limekuwa shirika la kihuduma..Mwelekeo wa kihuduma unaonekana, mambo mazuri yanakuja ndani ya miaka miwili, mitatu ijayo litakuwa shirika bora na lenye viwango bora la utoaji huduma na mwelekeo wetu unakwenda sambamba na bajeti ya wizara tuliyoitoa Bungeni kwa maslahi ya watanzania wote.'' Amesema Makamba.
Akifafanua juu ya kauli mbiu ya maonesho hayo ya 'Tanzania ni Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji' Makamba amesema, huduma wezeshi za uwekezaji ni pamoja na nishati ya umeme ya uhakika wakiwa kama sekta na watoa huduma hiyo (TANESCO,) wanafahamu wajibu wa kujenga mazingira ya kuvutia wawekezaji kwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suhulu Hassan za kuitangaza nchi ulimwenguni.
''Tunaunga mkono jitihahada zinazofanywa na Rais, sisi tunaosimamia sekta zinazovutia uwekezaji tupo tayari, TANESCO wana miradi mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa umeme ukiwemo mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere na miradi mingine ya kuhakikisha upatikanaji na usambazaji wa umeme ni wa uhakika... kazi tunazofanya zinasadifu kauli mbiu ya maonesho haya.'' Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO,) Maharage Chande amesema wamejipanga kuwa shindani katika bara za Afrika kwa kuzalisha umeme kwa kiwango cha juu na toshelevu kwa gharama himilivu za uzalishaji.
''Tuna miradi mingi ya kuhakikisha nishati ya umeme inakuwa ya uhakika ikiwemo mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere utakaotumia maji na mingine itakayotumia gesi, tunaamini kupitia miradi hii tutakuwa na umeme wa kutosha, bei himilivu na tutakuwa washindani katika ukanda wa Afrika.'' Amesema.
Chande amesema shirika hilo lenye mitambo ya umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1700 ina miradi ya umeme ya kuunganisha Tanzania na nchi nyingine katika Ukanda wa Afrika ikiwemo Kenya, Zambia na Msumbiji na uwepo wa gesi ya kutosha nchini utasaidia kuzalisha umeme mkubwa na kuweza kufanya biashara ya umeme kwa kushirikiana na nchi za ukanda.
''Tunahitaji muda na tunaamini tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuweza kuuza umeme katika nchi jirani, muda mfupi wa kuzalisha umeme ni miezi 24 tena ni umeme wa nishati jadidifu ya jua au upepo, na uzalishaji wa umeme wa maji huchukua takribani miezi 36, 42 hadi 60 tuna mipango na juhudi katika kuhakikisha tunafanikisha miradi ya namna hiyo kwa wakati ili tuwe shindani katika Kanda, taifa lifanikiwe kwa kuwa na nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu na kujenga uchumi imara.'' Amesema.
Waziri wa Nishati January Makamba akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda TANESCO na kueleza kuwa shirika hilo limekuwa likibadilika na kuwa la kihuduma zaidi na amewapongeza kwa jitihada za kukutana na wateja na kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi,Waziri wa Nishati, January Makamba akiwa ameambatna na Mkurugenzi mkuu wa TANESCO Maharage Chande wakiangalia gari linalotumia umeme wakati wa Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara, katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...