Na Beatrice Sanga MAELEZO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema wizara yake itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na kushirikisha Asasi za kiraia ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika kupata haki zao.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo leo, Julai 20, 2022 katika ofisi za Makao Makuu ya RITA, Jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ya wizara ya katiba na sheria ambapo ameeleza vipaumbele mbalimbali ambavyo Wizara hiyo imepanga kutekeleza katika huu wa fedha.
Dkt Ndumbaro amesema kuwa, moja ya mkakati ambao wizara imepanga kutekeleza katika mwaka wa fedha 2022/23 ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kikatiba na utawala wa sheria ili kusaidia wananchi kuwa na uelewa mpana ikiwa ni pamoja na kuelewa umuhimu wake katika kupata haki zao
“Wengi wanaongelea katiba lakini hawaijui na hawaielewi, ni lazima wananchi tuwape historia waelewe umuhimu wa katiba, lakini lazima tujue historia ya katiba hapa Tanzania. Wengi wanadhani kwamba hii ni katiba ya kwanza kwa Tanzania, lakini ukweli ni kwamba, Katiba hii nia Nne kwa Tanzania Bara na Katika Muungano hii ni katiba ya Pili,” alifafanua Dkt. Ndumbaro
Ameendelea kusema kuwa, kama wizara watashirikiana na Asasi zisizo za Kiserikali, ambapo wamejipanga kutoa elimu kwa Watanzania wote hasa wa ngazi ya chini walioko vijijini, kueleza mazuri na mabaya ili kuwapa wananchi uelewa wa kutosha juu ya katiba.
Vilevile amesema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23 wizara itatekeleza Programu ya kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji haki nchini ili kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya haki zao pale wanapotaka kushtaki, kushtakiwa au kupata uelewa juu ya haki zao
“Moja kati ya sababu watu hawazijui, ni sheria na haki zao, na hii ni kwa sababu sheria nyingi zilikuwa zimeandikwa kwa lugha ya kingereza sisi katika mwaka huu tunakwenda kusisitiza matumizi ya kugha ya Kiswahili katika mifumo yote ya utoaji haki. Tayari tumeshatafsiri sheria zaidi ya 220 kutoka kingereza kwenda kiswahili na sheria yoyote ambayo inatungwa kuanzia sasa na kuendelea ni lazima iwe na toleo la kiswahili” Amesema Dk Ndumbaro
Aidha Dkt Ndumbaro ameeleza vipaumbele vingine ambavyo wizara yake itaenda kutekeleza katika mwaka wa fedha 2022/23 ni pamoja na kuanza kujenga vituo jumuishi vya Taasisi za Sheria nchini, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria, kuendelea kuimarisha usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu pamoja na shughuli za ufilisi na udhamini, kurahisisha utatuzi wa mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu na kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majembo ya mahakama katika ngazi mbalimbali ili kurahisisha huduma za kisheria kwa wananchi
Wizara ya Katiba na Sheria katika mwaka wa Fedha 2022/23 ilipitishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi 272,768,278,800.00(Bilioni mia mbili sabini na mbili,milioni mia saba tisini na nane, laki mbili sabini na nane elfu na mia nane) kwa ajili ya Wizara na Taasisi zake ili kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya bajeti iliyopitishwa katika mwaka wa fedha 2021/22.
Home
HABARI
TUTASHIRIKISHA ASASI ZA KIRAIA KATIKA KUTOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU KATIBA NA SHERIA – DKT NDUMBARO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...