Na Said Mwishehe, Michuzi TV
KAMISHNA wa Bima nchini Dk.Baghoyo Saqware amewapongeza Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuamua kuungana na jitihada za Serikali kuendeleza soko la bima nchini.
Dk.Saqware ametoa kauli hiyo leo Julai 12,2022 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti katika sekta ya bima kuhusu mfumo wa fedha jumuishi ambapo amesema hatua ya UNDP kufadhili mchakato wa utafiti katika soko letu ni kuonesha utayari wao katika kuthamini umuhimu wa sekta ya bima katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Utafiti huu unaleta hamasa kwa Mamlaka na Serikali kwani matokeo na mapendekezo yake yanatoa chachu ya kuendeleza soko la bima kwa kuwa na taarifa sahihi.Ni wazi kuwa ukuaji na uchangiaji wa sekta ya bima katika pato la taifa bado uko chini.
“Hii ni kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kwa kutumia matokeo na mapendekezo ya utafiti huu niziase kampuni za bima kuandaa bidhaa bora na gharama zinazoendana na uhalisia na mahitaji ya soko. Hii itakuwa chachu ya kuendelea kusogeza huduma za bima karibu na wananchi.
“Pia ninawaomba UNDP kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Bima kufanya tafiti mbalimbali ili kubaini njia nzuri za kusambaza huduma na bidhaa za bima, njia nzuri ya kufadhi na kutoa bima kwa makundi yenye kipato cha chini pia namna sahihi ya kufanya soko la bima nchini kuwa himilivu,”amesema Dk.Saqware.
Ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia watafiti wote wote utayari wao kama Mamlaka ya bima nchini Tanzania kwa muda wowote kama kuna tatizo la aina yoyote linalohusu uendeshaji wa shughuli za bima walipeleke ili lipatiwe ufumbuzi kwa pamoja ili kuendeleza soko la bima.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNDP Christina Musisi ameeleza ripoti ya uchunguzi bima inalenga kufafanua hali ya mazingira kwa bima jumuishi na fedha za hatari nchini Tanzania pamoja na kuangazia fursa na matatizo.
“Ripoti hiyo itaangazia fursa ambazo UNDP na washirika wake wanaweza kunufaika nazo kupitia programu za usaidizi wa kiufundi katika miaka miwili hadi mitatu ifuatayo ili kuboresha mazingira ambayo yanaunga mkono bima sawa.Lengo ni kuunda na kutekeleza masuluhisho mahususi ambayo yanafaa kwa muktadha wa Tanzania.
“Kazi ya UNDP juu ya Bima na Ufadhili wa Programu kuu ya Bima na Ufadhili iliandaliwa na UNDP kama matokeo ya kupanua kazi yake katika eneo hili, na iliyoanzishwa hivi karibuni. Kitovu cha Sekta ya Fedha sasa kina kituo maalum cha kusaidia ofisi za kitaifa za UNDP na washirika wa nchi mbalimbali ulimwenguni kote. Kazi hii inashughulikia maeneo kadhaa muhimu liwekiwemo eneo la bima,”amesema Musisi.
Aidha amesema sekta ya bima inaweza kuchangia pakubwa katika kufikia na kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs.) na kwamba pamoja na mambo mengine UNDP itafanya kazi na nchi na jumuiya ili kuendeleza na kutoa ufumbuzi wa bima.
Pia kushirikiana na washirika kubadilisha masoko ya bima kupitia sheria iliyoboreshwa, udhibiti, na uwezo wa taasisi. “Matokeo ya kazi hii ya uchunguzi yatatumika kuandaa programu ambazo zitasaidia kuboresha mazingira wezeshi ya Tanzania kwa bima shirikishi.
“UNDP ilianza shughuli zake nchini Tanzania baada ya kutiliana saini Mkataba wa Msaada wa Kawaida wa Msingi (SBAA) na Serikali tarehe 30 Mei 1978. Lengo kuu la UNDP Tanzania ni kuisaidia Serikali ya Tanzania kuboresha maisha ya watu kupitia maeneo ya kimkakati ya kidemokrasia. utawala, ukuaji wa uchumi shirikishi na maisha endelevu na uendelevu wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu.”
Wakati wa uzinduzi huo imeelezwa kwamba dhamira ya TIRA ni Kukuza, kudumisha umoja, ufanisi, haki na usalama. na soko thabiti la bima kwa manufaa na ulinzi wa wamiliki wa sera
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa(UNDP) Christina Musisi akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa utafiti katika sekta ya bima kuhusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Bima Dk.Baghayo Saqware akizungumza mbele ya wadau wa sekta ya bima nchini wakati wa uzinduzi ripoti ya utafiti katika sekta ya bima kuhusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Bima Dk.Baghayo Saqware (wa kwanza kulia) akiandika jambo wakati wa uzinduzi wa utafiti huo uliotolewa na UNDP kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA).
Kamishna wa Bima Dk.Baghayo Saqware akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kutoka sekta za bima, serikali , maofisa kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Matifa(UNDP) pamoja na wadau wengine wakiwa katika picha baada ya kuzinduliwa kwa ripoti ya utafiti katika sekta ya bima kuhusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa uzinduzi wa utafiti huo uliohusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu washiriki waliohudhuria uzinduzi huo wakifuatilia mijadala mbalimbali kabla ya kuzinduliwa kwa ripoti ya utafiti kuhusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Utafiti huo umefanyika kwa ushirikiano kati ya UNDP na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA).
Sehemu ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo ripoti ya utafiti katika sekta ya bima kuhusu mifumo ya fedha jumuishi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...