Sehemu ya Kiwanda kidogo cha kusindika mafuta ya alizeti cha Kishapu mkoani Shinyanga
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi
wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti cha Kishapu, Eliudy
Humphrey Urassa amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kilimo cha
alizeti ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya alizeti
ikiwa ni sehemu kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta kwani
viwanda vya kusindika mafuta vipo.
Akizungumza
na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania
waliotembelea kiwanda chake kilichopo Mhunze wilayani Kishapu Julai
14,2022, Urassa amesema vipo viwanda vikubwa na vidogo vinavyosindika
mafuta yatokanayo na mazao kama chake mkoani Shinyanga ambavyo ni
suluhisho la kukabiliana na adha ya uhaba wa mafuta nchini.
“Katika
Kiwanda chetu cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil tunatengeneza
mafuta ya asili ya alizeti, mafuta haya hayana kemikali, tunatumia njia
za asili kusindika mafuta haya ambapo kwa siku kiwanda hiki kidogo
kinazalisha tani moja hadi moja na nusu. Tunashukuru wananchi wengi
wanatupa ushirikiano wa kununua mafuta yetu ndani na nje ya wilaya ya
Kishapu.
Kwa
kweli tumesaidia kupunguza changamoto ya mafuta, Tunauza mafuta kwa bei
ya jumla na rejareja kwa bei nafuu sana hata mwananchi akija na
kifungashio chake tunamuuzia, bei zetu ni rafiki. Tunauza mafuta hadi
lita 20 na tumefanya ubunifu tunavyo vipimo hadi vya shilingi 1000 ili
kumwezesha kila mwananchi kutumia mafuta haya”,amesema Urassa.
Urassa
ameiomba serikali kuleta mbegu bora iwapatie wananchi ili waweze
kuzalisha kwa wingi kwa vile wilaya ya Kishapu ina wakulima wengi wa zao
la alizeti na kuhamasisha wananchi kulima mazao yanayotoa mafuta
ikiwemo alizeti na pamba ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha
mafuta ili kuondokana kabisa na uhaba wa mafuta.
Ametumia
fursa hiyo kuiomba Serikali kupitia Mawaziri husika kumpatia nafasi ya
kwenda kujifunza masuala ya viwanda nje ya nchi ili kujifunza
wabadilike, waongeze maarifa na kuboresha zaidi kiwanda chake hicho
kidogo alichokianzisha mwezi Juni,2021 ili kutoa ajira zaidi kwa vijana
na sasa wanauza mafuta kwa bei nafuu na kusafirisha mashudu nje ya nchi
ikiwemo Rwanda.
Afisa
Kilimo wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Kitundu amesema katika
wilaya ya Kishapu wapo wajasiriamali wadogo akiwemo Urassa ambao
wameanzisha viwanda vidogo vya kusindika mafuta na sasa wanaendelea
kuhamasisha wananchi kulima mazao yanayotoa mafuta ikiwemo alizeti na
pamba ili viwanda vinavyoanzishwa vipate malighafi na kuondoa uhaba wa
mafuta na kushusha gharama za maisha.
Mkuu
wa wilaya ya Kishapu, Joseph Modest Mkude amewapongeza wajasiriamali
walioanzisha viwanda vidogo vya kusindika mafuta wilayani Kishapu
ambavyo vinapunguza tatizo la upatikanaji mafuta.
“Mwitikio
wa kilimo cha zao la alizeti wilayani Kishapu ni mkubwa sana, wananchi
wamejitokeza kulima na wengine wameanzisha viwanda vidogo vya kukamua
mafuta ya alizeti. Mafuta haya yana nembo ya Kishapu. Sisi kilimo ni
biashara, tunalima hapa tunachakata mafuta hapa na kupata bidhaa hapa.
Tunachohitaji sasa ni kuwa na vifaa bora zaidi vya kukamua mafuta yote
ili kupata mafuta mengi zaidi kwani vifaa vilivyopo kuna mafuta
yanapotea”,amesema Mkude.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson amesema katika msimu huu
wananchi wamelima zao la alizeti na pamba kwa wingi na wataendelea
kuhamasisha wananchi kulima kila zao kwani kipaumbele chao katika
halmashauri hiyo ni kilimo.
“Tunawahamasisha
kujihusisha na kilimo kwani kilimo siyo adhabu, hakuna zao ambalo
halina soko, vijana walime ili kujiletea maendeleo na sisi tutaendelea
kuwajengea uwezo wananchi walime kwa tija ili wavune kama
walivyokusudia. Kilimo ni biashara”,amesema Johnson.
Nao
wakulima wa zao la alizeti akiwemo Nyorobi Kasema na Jiyenze Seleli
wamesema kiwanda hicho kidogo kimesaidia kupunguza adha ya mafuta kwa
wananchi licha kununua mafuta lakini wengi wanapeleka alizeti yao kwenda
kusindika na kupata mafuta ya kutumia majumbani mwao.
Mkurugenzi
wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold
Sunflower cooking oil mkoani Shinyanga Eliudy Humphrey Urassa akielezea
namna kiwanda chake kidogo kinavyosaidia kukabiliana na tatizo la
upatikanaji mafuta nchini. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Afisa
Kilimo wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Kitundu akizungumza ndani ya
Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold
Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano
wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta
ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano
wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta
ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano
wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta
ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson akielezea fursa mbalimbali
zinazotokana na kilimo na kuwataka vijana kuchangamkia fursa katika
Kilimo.
Mkuu
wa wilaya ya Kishapu, Joseph Modest Mkude akielezea faida ya viwanda
vidogo wilayani Kishapu na kupongeza wananchi walioanzisha viwanda vya
kusindika mafuta ya alizeti.
Mkulima wa alizeti Jiyenze Seleli akielezea namna viwanda vidogo vinavyosaidia kupunguza adha ya mafuta.
Mkulima wa alizeti Nyorobi Kasema akielezea namna viwanda vidogo vinavyosaidia kupunguza adha ya mafuta.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...