Afisa Udhibiti Ubora wa Bodi hiyo, Witness Temba akizungumza na Michuzi TV kwenye Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema idadi kubwa ya Wakulima wa mazao mbalimbali nchini wamenufaika na mfumo wa Stakabadhi za Ghala kupitia bei za mazao yao.
Hayo yameelezwa na Afisa Udhibiti Ubora wa Bodi hiyo, Witness Temba kwenye Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Temba amesema kuna manufaa yanayotokana na kugundua bei bora zaidi ya mazao hayo.
Pia amesema uzalishaji wa mazao umeongezeka kutokana na mfumo huo wa Stakabadhi za Ghala. Amesema mfumo unawanufaisha pia Wanunuzi wa mazao hayo kutokana na kupata bidhaa inayohitajika kwa wingi na kwa wakati na zenye ubora.
“Utaratibu wa Mnada wa mazao unakuwa na ushindani zaidi, unapatikana uvumbuzi wa bei zenye tija kwa Wakulima, mfano zao la Korosho kumekuwa na kuimarika kwa bei msimu hadi msimu, kutokana na matumizi ya mfumo wa Stakabadhi za Ghala”.
“Mfano zao la Kakao kule Kyera, mkoani Mbeya na hata Mvomero, mkoani Morogoro kuna tofauti kubwa ya mauzo ya mazao kabla ya mfumo na baada ya mfumo, bei zimekuwa na tija na ongezeko ambalo ni kubwa sana kwa Wakulima”, amesema Temba.
Bodi hiyo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na lengo la Urasimishaji wa Biashara, hususani kwenye mazao ya Kilimo, Pia Bodi hiyo imepewa Mamlaka ya kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...