Na. Veronica Mwafisi - Babati
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Walengwa wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini kuboresha maisha yao kupitia ruzuku wanayopewa ili kuunga mkono azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini alipokuwa akizungumza na walengwa hao wa Mtaa wa Arri waloiopo Kata ya Nangara Babati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango huo katika Halmashauri ya Mji wa Babati.
Mhe. Ndejembi amewataka walengwa kujiuliza namna Mhe. Rais anavyojitoa katika kutoa fedha ili kuzikwamua kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwani angeliweza kuzielekeza fedha hizo katika shughuli nyingine za maendeleo.
“Mnaopokea ruzuku ya TASAF, ni jukumu lenu kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mnazitumia vema fedha za ruzuku katika kuboresha maisha yenu kama alivyokusudia,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amekemea kitendo cha walengwa wa TASAF kutumia ruzuku wanayopewa katika anasa kama vile kunywa pombe, jambo ambalo ni kinyume na lengo la Serikali la kuanzisha Mpango huo wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini.
Kwa upande wake mmoja wa walengwa wa TASAF wa Mtaa wa Arri kata ya Nangara Halmashauri ya Mji Babati, Bi. Lyidia Kaaya amesema ruzuku ya TASAF imemuwezesha kuboresha maisha yake kwani alianza kufuga kuku na baadae kukodi shamba kwa ajili ya kilimo na alipovuna aliuza mazao na kupata fedha zilizomuwezesha kujenga nyumba anayoishi hivi sasa.
Naye, Mlengwa mwingine Bi. Hellena Philemon ameishukuru TASAF kwa kumboreshea maisha yake, ambapo amewezeshwa kusomesha watoto na kuboresha nyumba yake kwani kabla ya kuanza kupokea ruzuku hakuweza kumudu gharama za masomo na kukarabati nyumba yake.
Aidha, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Oscar Maduhu amesema kuwa, TASAF imeona mafanikio makubwa ya walengwa wengi waliotumia ruzuku vizuri kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi, na wapo wachache wanaosuasua hivyo TASAF inaendelea kutoa elimu ya namna bora ya kutumia ruzuku ili kuboresha maisha yao.
Bw. Maduhu amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan bado anaendelea kutoa fedha za kutosha kuwezesha Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini, hivyo TASAF itaendelea na uratibu wa kuhawilisha kwa utaratibu wa mpango ili ziwafikie walengwa waliokusudiwa.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakimshukuru, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuboresha maisha yao kupitia ruzuku inayotolewa na TASAF.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...