Na Mbaraka Kambona, Pwani

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali haitavumilia vitendo vya uingizwaji wa vifaranga vya kuku kwa njia za panya hapa nchini kwa sababu vinasababisha nchi kukosa mapato na kufubaza jitihada za uwekezaji nchini.

Ulega alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani alipotembelea mashamba ya kutotoleshea vifaranga vya kuku ya Organia na Mkuza Chicks aliyoifanya Julai 11, 2022.

 Akizungumza na wawekezaji wa mashamba hayo kwa nyakati tofauti, Waziri Ulega alisema  kuwa kuanzia sasa Wataalamu waliopo Wilayani na katika mipaka yote ya nchi watakuwa makini kufuatilia kwa karibu na wale wote wanaoingiza vifaranga kiholela na wakabainika watawajibishwa.

"Hawa watu wanaoingiza vifaranga kienyeji bila kufuata sheria, taratibu na kanuni zetu sio tu wanasababisha nchi kukosa mapatoa bali wanaangusha uwekezaji wa ndani ya nchi na uchumi kwa ujumla", alifafanua

Ili kukabiliana na vitendo hivyo, Waziri Ulega aliwaelekeza Wataalamu wanaohusika na usimamizi wa vibali vya kuingiza vifaranga kuandaa mfumo madhubuti utakaokuwa na taarifa zitakazowezesha serikali kujua na kusimamia vizuri zoezi hilo la utoaji vibali.

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri sana ya kualika wawekezaji nchini, sasa ni kazi yetu kila mmoja kulinda uwekezaji wa namna hii",alisema

Aidha, alitumia fursa hiyo pia kuwaomba Wafugaji wa kuku nchini kuziamini kampuni zinazozalisha vifaranga hapa nchini huku akiongeza kuwa kama kuna changamoto yoyote inayotokana na wazalisha hao basi wasisite kuziwasilisha Wizarani ili zifanyiwe kazi kwa lengo la kuboresha huduma hiyo.

"Lakini vilevile tunaponunua vifaranga vya hapa nyumbani inasaidia kukuza uchumi wetu, kuweka usalama wa uwekezaji tunaowaalika kuja kuwekeza hapa nchini," aliongeza

Awali, wawekezaji wa Mkuza Chicks na Organia walimueleza Naibu Waziri huyo  kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uingizwaji holela wa vifaranga kutoka nje jambo ambalo linasababisha biashara hiyo kutokuwa ya uhakika.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa kwanza kushoto) akipatiwa maelezo kuhusu kifaa kinachoonesha ukuaji wa kifaranga ndani ya yai mpaka siku kitakapototolewa alipotembelea shamba la Ogania lililopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Julai 11, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akionesha sehemu ya vifaranga  vinavyozalishwa katika shamba la kutotoleshea vifaranga vya kuku la Ogania lililopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani alipotembelea shamba hilo Julai 11, 2022. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sara Msafiri. Wengine ni viongozi wa shamba hilo la Organia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...