Na Okello Thomas-GCLA
Madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi wametakiwa kupata elimu ya usimamizi na usafirishaji salama wa kemikali hatarishi pamoja na kufuata kanuni na sheria za usafirishaji wa kemikali nchini.
Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, alisema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya madereva 140 wanaosafirisha mizigo ya kemikali yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.
“Wasafirishaji wote wa kemikali hatarishi mnatakiwa kisheria kuwa na vibali vyote Mkemia Mkuu wa Serikali ambavyo vinahitajika wakati wa kusafirisha kemikali na kuhakikisha kemikali inasafirishwa kwa usalama na dereva awe amepitia mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali ili kuondokana na athari pale inapotokea majanga wakati wa usafirishaji wa kemikali,” alisema Elias.
Pia Mkurugenzi alibainisha kuwa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali, yatolewe kwa wamiliki wa magari na makampuni kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya faida ya kuwapeleka madereva na wasimamizi wa kemikali kupata elimu hiyo na kuelewa changamoto zinazowakabili madereva pindi wanaposafirisha kemikali na namna ya kuzitatua.
Aidha, aliwasisitiza madereva kuzingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa kemikali hatarishi ili kuepusha kuleta madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, amewasihi madereva kufahamu na kutambua aina ya kemikali wanayosafirisha ili kuweza kuchukua tahadhari kabla na wakati wa kusafirisha kemikali kwani usafirishaji wa kemikali unahitaji umakini mkubwa.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Ali Mhina, dereva kutoka kampuni ya Tazama Pipe Line ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa kutoa mafunzo kwa madereva kwani mafunzo humjenga dereva kwa kujitambua, kuwa makini pamoja na kuitambua jamii.
“Tunaipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutambua umuhimu wa afya na usalama wa dereva na kuhakikisha dereva anasafirisha kemikali kwa usalama, mafunzo haya yatatusaidia katika kusafirisha mizigo ya kemikali kwa usalama mkubwa ukilinganisha na tulivyokuwa tunaifanya kazi hii kabla ya mafunzo haya” alisema Ali.
Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), David Elias (aliyesimama), akisisitiza jambo kuhusu usafirishaji salama wa kemikali hatarishi kwa madereva wakati akifunga mafunzo ya madereva wanaosafirisha kemikali yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi Kanda ya Mashariki. Mafunzo haya ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa Maaskofu Kurasini, jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya madereva 140 wamehudhuria mafunzo hayo.
: Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), David Elias (kushoto), akimkabidhi cheti cha ushiriki mmoja wa madereva waliohudhuria mafunzo ya madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi Kanda ya Mashariki. Mafunzo haya ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa Maaskofu Kurasini, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo zaidi ya madereva 140 wamehudhuria mafunzo hayo.
Mmoja wa madereva waliohudhuria mafunzo ya madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi, akiwasilisha mada katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi Kanda ya Mashariki. Mafunzo haya ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa Maaskofu Kurasini, jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya madereva 140 wamehudhuria mafunzo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...