Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala ameagiza kusitishwa kwa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango katika Mkoa wake kwani vifungashio hivyo vimekuwa chachu ya uchafuzi wa mazingira katika Mkoa huo pale vinapotumiwa na Wananchi katika masoko kama mifuko ya kubebea bidhaa badala ya kutumika kama vifungashio.
Ameyasema hayo Ofisini kwake wakati wa kikao kazi baina yake na Wadau wengine kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kama vile Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC), Shirika la kudhibiti ubora na viwango Tanzania (TBS), Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na Wawekezaji wanaojishughulisha na uzalishaji wa mifuko mbadala (non-woven) kwa lengo la kujadiliana masuala ya matumizi sahihi ya vifungashio vya plastiki na mstakabali mzima wa mazingira.
“Naelekeza kikosi kazi kuanza operesheni katika mkoa wa Dar es Salaam ya kuondoa vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango ambavyo imegeuzwa kuwa mifuko ya kubebea bidhaa katika masoko yote”.
Aidha ameiagiza NEMC kuandaa kikao na Wenyeviti na Makatibu wa Masoko katika mkoa wa Dar es Salaam ili kuwapa elimu kuhusiana na matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango katika maeneo ya masoko katika Mkoa huo.
Ameongeza kuwa baada ya kikao hiko NEMC ianze oparesheni ya kutokomeza vifungashio hivyo vya plastiki visivyokidhi viwango mara moja na wote wanaotumia vifungashio hivyo visivyokidhi viwango wachukuliwe hatua za kisheria.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka akiongea katika kikao hiko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa na kuwapa Nemc ushirikiano katika kutokomeza kero hiyo ya matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango ambavyo hutumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni. Amewaomba na Wakuu wengine wa Mikoa kuiga mfano huo ili kuweza kurahisisha zoezi hilo la kutokomeza vifungashio visivyokidhi viwango.
Aidha ameainisha changamoto NEMC wanazokutana nazo katika kutokomeza vifungashio vya plastiki visiyokidhi viwango ikiwemo njia za panya za uingizaji wa mifuko hiyo, pia kupata ushirikiano mdogo kutoka serikali za mitaa kuanzia ngazi ya chini kabisa kwani NEMC peke yake hawawezi. Ameongeza kuwa NEMC itaendelea kutoa elimu kwa jamii pamoja na wafanyabiashara kuhusiana na matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango. Mwisho amemuahidi Mkuu wa Mkoa kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa kwa NEMC.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Udhibiti wa viwango kutoka TBS, Bwana Lazaro Henry Msasalaga amesema Shirika la Viwango liko tayari kushirikiana na NEMC kama walivyofanya awali ili kuweza kutokomeza vifungashio hivi visivyokidhi vilivyozagaa katika masoko.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Al Hasseeb l.t.d, Bwana Hassan Tariq wanaozalisha mifuko mbadala maarufu kama non woven bags ameiomba Serikali kudhibiti wimbi hili la vifungashio visivyokidhi viwango ambayo hutolewa sokoni bure kwa wananchi na hutumika kama mifuko ya kubebea bidhaa. Kwani wao kama wazalishaji wa mifuko mbadala wanapata hasara sababu mifuko hiyo hainunuliwi tena.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Amos Makala akiongea wakati wa kikao kazi na Wadau kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo NEMC kuhusiana na kutapakaa kwa vifungashio vya plastiki ambavyo vinatumika kama mifuko ya kubebea bidhaa katika mkoa wa Dar es Salaam.
Sehemu ya Wadau walioshiriki kikao kazi hiko kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Amos Makala.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka pamoja Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira kutoka NEMC Injinia Redempta Samuel wakifuatilia maelekezo yaliokua yakitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama Mheshimiwa Amos Makala katika kikao hiko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...