Jophillen Bejamulla( kushoto) kutoka C40- Cities akifuatilia jambo kwenye laptop wakati wa kikao hicho.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MUUNGANO wa wa AZAKI za Uchechemuzi wa Huduma za hali ya hewa unaoratibiwa na Can Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadiliana namna ya kuboresha mahusiano yanayowezesha mtiririko wa taarifa za huduma za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania mpaka kwa mtumiaji wa mwisho.
Mbali ya taarifa kufika kwa mtumiaji wa mwisho pia kutoa mrejesho wa uboreshaji wa nyenzo na mchakato wa upatikanaji wa huduma za hali ya hewa.
Muungano huo unaoratibiwa na AZAKI ya CAN Tanzania upo chini ya mradi wa “Maendeleo endelevu yanayozingatia makabiliano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya nishati jadidifu” unaofadhiliwa na Shirika la Kijerumani la Brot für die Welt.
Wakizungumza leo Agosti 25,2022 kwenye majadiliano hayo wadau wa Muungano huo pia wamejadili mchango wa AZAKI katika uhamasishaji wa upatikanaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kama nyezo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha wamekaa na kujadiliana namna za kuboresha mahusiano yatakayowezesha mtiririko wa huduma za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania mpaka kwa mtumiaji wa mwisho wa taarifa na kutoa mrejesho wa uboreshaji wa nyenzo na mchakato wa upatikanaji wa huduma za hali ya hewa.
Pamoja na hayo wadauo hao kupitia mkutano huo wameazimia kuboresha mahusiano, kuimarisha michakato na kuongeza matumizi ya Huduma ya hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kama kilimo, ufugaji na uvuvi.
Aidha wadau hao wameeleza changamoto kubwa ipo kwenye mfumo wa mtiririko wa taarifa kuwafikia watumiaji wa mwisho kwa wakati kwani mfumo wa mtiririko wa taarifa za huduma ya hali ya hewa una protokali(urasimu) ndefu ambayo inawahusu watu wenye uelewa mdogo na tofauti juu ya mabadiliko ya tabianchi.
Wamesema hiyo inasababisha ucheleweshwaji na ufinyu wa matumizi huduma za hali ya hewa kwa wakati na hivyo kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha changamoto nyingine ni uchache wa rasilimali za kuboresha mchakato na ufikiaji wa taarifa hizo kwa wadau ili kuwezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta maendeleo endelevu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...