Na Fredy Mshiu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imefanya mkutano na wananchi wa mtaa wa Kisanga kata ya Wazo wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma ya maji waliyoanza kuipata kwa mara ya kwanza.
Kupitia mradi wa uboreshaji huduma kutoka Makongo hadi Bagamoyo takribani wakazi 200 wa mtaa wa Kisanga wameanza kupata huduma ya maji kwa mara ya kwanza pamoja na maeneo yaliyokuwa na msukumo mdogo wa maji kuimarika.
Akizungumza na wananchi katika mkutano huo Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Mivumoni Mhandisi Felchesim Kimaro ameeleza kuwa sasa neema imewafikia wananchi wa Kisanga na shida waliyoipata kwa muda mrefu ya kukosa huduma sasa imekwisha .
"Napenda kuwaambia wananchi wa Kisanga kuwa maji yamefika mtaani kwenu , mkandarasi anaendelea na kazi ya maunganisho kwa wananchi na wengi wameshaanza kupata huduma, niwahakikishie wakazi wote wa Kisanga mtapata huduma ya majisafi," ameeleza Mhandisi Kimaro.
Mhandisi Kimaro ameongeza kuwa DAWASA imejipanga kuhakikisha wananchi wote waliopo nje ya mita 50 kutoka bomba kubwa wanapata huduma ya maji bila kuachwa, huku akiwaomba kutoa ushirikiano pindi wanapohitajika kutoa maeneo ya kupitisha bomba kwa ajili ya kusogeza huduma.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Wazo ndugu, Lenard Manyama ameishukuru DAWASA kwa kuwapatia wananchi wa Kisanga elimu nzuri juu ya huduma wanazotoa.
"Niwashukuru sana DAWASA kwa kufika, mmekua wepesi kuja kuongea na wananchi, niwapongeze kwa hilo, kwa sasa tunaweza kupata usingizi kwa kuwa uhakika wa maji upo," ameeleza ndugu Manyama.
Ndugu Manyama amewaomba wananchi wa Kisanga kutoa ushirikiano na kutokung'ang'ania ardhi pindi Mkandarasi anapotaka kupitisha bomba kuhudumia wananchi huku akiagiza kila mjumbe wa shina kuhakikisha wananchi wake wanapata maji kwa kushirikiana na DAWASA.
Ndugu Esther Mwakimbwala mkazi wa mtaa wa Kisanga ameshukuru kwa jitihada zilizofanyika na Serikali kupitia DAWASA mpaka sasa wanapata maji katika mtaa wao jambo ambalo mwazoni walidhani halitawezekana.
Mradi wa kuboresha huduma ya maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wakazi 450,000, ukihusisha ujenzi wa matenki 3 katika maeneo ya Vikawe, Mbweni na Tegeta A yenye ujazo wa lita milioni 5 kila mmoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...