Imeandikwa na Bashir Yakub, WAKILI - +255 714 047 241.
Tatizo ni vyuo vya sheria. Tatizo linaanza na sifa za udahili wa wanafunzi wanaostahili kusomea sheria katika vyuo, na Pili mfumo wa ufundishaji vyuoni.
Kuna vyuo hadi mwenye D flat, D English, D kiswahili na D history anapata na nafasi ya kusoma sheria.
Sasa hivi karibia hamna chuo hakitoi degree ya sheria. Chuo hata kikiwa kipya moja ya kozi ambazo wanaanza nazo na ya sheria lazima iwemo.
Mchanganyiko huu hauwezi kuwa salama ukifika Law School ambapo maadili na taaluma ya sheria inasimamiwa kwa uthabiti.
Hatusemi vyuo vya sheria visiwe vingi ama watu wasidahiliwe kwa wingi, tunazungumzia ubora wa vyuo hivyo katika kutoa taaluma hiyo, na ubora wa wadahiliwa wenyewe.
Niwaambie kitu, asilimia 90 ya wanafunzi wanaomaliza sheria katika vyuo vyetu hawawezi hata kuandaa kiapo(affidavit). Kiapo tu.
Simsingizii mtu, mahakimu na mawakili mnaokaa na wanafunzi hao wakija field mnajua na mmekuwa mkikilalamika sana kuhusu hili.
Nazungumzia kiapo wala sizungumzii kuandaa mashitaka(Plaint au Charge) au utetezi( Wsd), kiapo tu hawajui.
Mtu kama huyu unataka Law School iseme amefaulu, ili akafanye nini mtaani. Akatoe huduma gani.
Kuna kitu jamii inapaswa kuelewa. Law School haizalishi tu Mawakili bali Mahakimu na Majaji. Tokea ilipoanzishwa hawi mtu Hakimu ama Jaji isipokuwa amefaulu Law School.
Unaonaje mtu kama Jaji ama hakimu mwenye mamlaka ya kuhukumu mtu kunyongwa hadi kufa, kuhukumu kifungo cha maisha jela, kifungo cha miaka 30, kuhukumu upoteze nyumba ama mali yako nk awe mtu aliyefaulu kiujanjaujanja tu ilimradi. Haiwezekani
Law School inahiaji watu "Pure" na wala haimuonei yeyote. Inahitaji watu ambao watabeba majukumu mazito kama hayo niliyoainisha hapo juu.
Hayo majukumu ni mazito sawa na ya udaktari. Ni majukumu ambayo mstari wake ni kati ya kifo na uhai.
Wanafunzi wenyewe wanajua na ndio maana wakifeli wanakimbilia kwenye media. Zipo taratibu za rufaa kwa waliofeli lakin hawataki kuzitumia sababu wanajua hawatatoka kutokana na ukweli. Wanajua kabisa wamefeli kwasababu hawajaiva inavyostahili.
Na suala la kuhakikisha Wakili anaiva vizuri kabla ya kuapishwa halijaanza na Law School. Lilikuwepo hata kipindi cha Bar Exam kabla Law School haijaanzishwa. Mwendo ulikuwa huu huu. Waulizeni waliopitia mfumo huu wa Bar Exam watakuelezeni. Mtu alikuwa akirudia mitihani hii hata mara 15 ili aweze kufaulu na kuapishwa kuwa Wakili.
Lengo ni hilohilo kumuandaa mtu sahihi atakayebeba haya majukumu mazito ya kifo na uhai.
Kwa ufupi, kama kuna sehemu ya kushugulikia kuondokana na kadhia hii ni vyuo vya Sheria. Mifumo ibadilike kuanzia sifa za udahili hadi ufundishaji.
Sifa za udahili wa shetia zimeshushwa mno, Pili Wajitoe katika kufundisha Theory na wajikite katika Practical. Law is about practise 80% and theory 20%.
Tusitafute mchawi Law School. Na ukitaka kujua ukweli wa hili ni nadra mno tena mno mtu ambaye amemaliza chuo akapractise kwa muda aidha kwa mawakili au mahakamani then akaenda Law School, kumkuta amefeli.
Hao wachache mnaosikia wanafaulu wengi sio fresh from school. Ni watu ambao wametoka ofisi za mawakili au wamepractise mahakamani.
Hawa wa kutoka chuo moja kwa moja Law School hufeli karibia wote, itokee tu.
Kwahiyo ni muhimu kuangalia hayo mambo mawili, Kwanza sifa za udahili wa wanafunzi ambao wanatakiwa kusomea sheria, Pili mfumo wa vyuo ubadilike kutoka theory na kuwa practical zaidi.
Tuachane na Law School iandae watu Mahiri. Tunahitaji watu mahiri wabebe majukumu mazito ya kifo na uhai.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...